Iran yalaani hujuma ya Marekani dhidi ya Yemen, yamuonya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i124060-iran_yalaani_hujuma_ya_marekani_dhidi_ya_yemen_yamuonya_trump
Iran imekemea kwa nguvu madai ya hivi karibuni yaliyotolewa na viongozi wa juu wa utawala wa rais wa Marekani Donald Trump na kuyataja kuwa ni "yasiyo na msingi" kabisa huku ikilaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya Yemen. 
(last modified 2025-03-18T04:23:45+00:00 )
Mar 18, 2025 04:23 UTC
  • Iran yalaani hujuma ya Marekani dhidi ya Yemen, yamuonya Trump

Iran imekemea kwa nguvu madai ya hivi karibuni yaliyotolewa na viongozi wa juu wa utawala wa rais wa Marekani Donald Trump na kuyataja kuwa ni "yasiyo na msingi" kabisa huku ikilaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya Yemen. 

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saied Iravani, alitoa kauli hii Jumatatu kwa njia ya barua kwa Katibu Mkuu wa UM na mwenyekiti wa Baraza la Usalama.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema: Ningependa kueleza wasiwasi wangu wa kina na kukemea vikali kauli za kivita za hivi karibuni kutoka kwa viongozi wa juu wa utawala wa Marekani, ikiwa ni pamoja na rais wa Marekani, wakati walijaribu kwa nguvu zote kutetea hujuma na uhalifu wa kivita dhidi ya Yemen, ambapo wametoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutishia wazi kutumia nguvu dhidi ya Iran." 

Kwa uchache watu 53, haswa wanawake na watoto, waliuawa na 101 waliujeruhiwa baada ya Marekani kufanya mashambulio ya kwanza dhidi ya Yemen tangu Trump aingie madarakani Januari.

Trump, katika taarifa yake ya Jumamosi, alisema kuwa Marekani inaitazama Iran “kuwa inabeba dhima kamili” kwa kuunga mkono harakati ya muqawama ya Ansarullah ya Yemen. Alisema eti 'msaada kwa harakati hiyo lazima “ukome mara moja."

Iravani amesema kuwa kauli za viongozi wa Marekani zinazopinga Iran ni ukiukaji wa wazi wa kanuni za msingi za sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Iravani ameonya kuwa kitendo chochote cha hujuma dhidi ya Iran kitakuwa na matokeo mabaya, ambayo Marekani itabeba dhima yake kamili. Naye Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameonya kwamba, Iran itatoa jibu la maangamivu kwa tishio lolote iwapo litatekelezwa kivitendo dhidi ya taifa hili.

Ameeleza bayana kuwa, Iran haina nafasi yoyote katika kuundwa na kuongoza sera za makundi ya Muqawama ya kieneo, ikiwa ni pamoja na Harakati ya Ansarullah ya Yemen.

Aidha Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, tishio lolote litakalotekelezwa dhidi ya Iran litakabiliwa na jibu kali, zito na la uharibifu.