Pezeshkian: Jeshi ni ngome imara ya serikali na taifa la Iran
Rais wa Iran amelitaja jeshi la Iran kuwa ni ngome imara ya serikali na taifa, chanzo cha heshima ya taifa, ni msaada kwa taifa na serikali.
Rais Masoud Pezeshkian amesema hayo leo katika maadhimisho ya Siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kwamba: Jamii itasalia katika hali ya usalama na utulivu iwapo jeshi litakuwa imara na kuwa tayari; na usalama ungetoweka katika jamii yetu kama nguvu hii iliyobarikiwa isingekuwepo katika jamii
Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa: Kuwepo kwa jeshi imara na lililoandaliwa vyema kumeiwezesha Iran kutekeleza kwa nguvu sera zake za kuanzisha uhusiano, amani na utulivu katika eneo hili.
Ameongeza kuwa: Iran imejiarifsha kama nchi yenye nguvu isiyo na mpinzani katika eneo hili kwa msaada wa vikosi vya ulinzi, polisi na vikosi vya usalama.
Pezeshkian ameashiria silsilaha na nafasi ya jeshi na kusema: Mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu maadui walijaribu kulidhoofisha jeshi, hata hivyo kutokana na kuwepo Kiongozi wa Mapinduzi jambo hilo halikutokea, na jeshi lilisalia imara na lilitoa vitani mashahidi zaidi ya elfu 48 na majeruhi laki mbili kwa utawala wa Kiislamu na nchi hii.

Akisisitiza kwamba mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu, nchi iliitegemea wageni katika masuala ya silaha za kijeshi, amesema: "Tulikuwa tegemezi kwa maadui wetu kwa ajili ya kutupa na kununua zana rahisi zaidi za ulinzi, lakini hii leo tunajivunia kwamba jeshi letu lenye nguvu limepata maendeleo makubwa katika kutengeneza zana zote za kijeshi na ulinzi zinazohitajika na nchi angani, nchi kavu, baharini, na katika utengenezaji wa vifaa vyote makini."