Baghaei: Russia ina mchango athirifu katika mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Russia ina nafasi na mchango athirifu katika kushughulikia faili la nyuklia la Iran.
Esmail Baghaei amekadhibisha ripoti za vyombo vya habari kuhusu Saudi Arabia kuwa mpatanishi katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington na kusema: Taarifa zote hizi ni uvumi na tetesi za duru za habari na hazina ukweli wowote.
Wakati huo huo Baghaei ameeleza kuwa katika siku zijazo Russia itaendelea kutekeleza wajibu wake muhimu katika kadhia ya nyuklia ya Iran na kwamba hivi sasa mazungumzo kati ya Iran na Marekani yako katika awamu ya kwanza; na nchi mbili bado hazijaingia kwa undani katika mazungumzo kuhusu kadhia ya nyuklia.
Awali shirika la habari la Novosti liliripoti kwamba Sauudia ina nafasi ya upatanishi katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington.
Duru ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani ilifanyika Jumamosi iliyopita Aprili 19 katika mji wa Roma nchini Italia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa takwa kuu la Iran ni kuondolewa vikwazo vilivyo kinyume naa sheria vyenye athari za kiuchumi, na kwamba: "Mazungumzo yaliendelea katika hali nzuri na yamepangwa kuendelea katika ngazi ya wataalamu kuanzia kesho Jumatano huko Oman."
Duru ya tatu ya mazungumzo ya Iran na Marekani imepangwa kufanyika Jumamosi ijayo Aprili 26.