Safari ya siku moja ya Rais wa Iran nchini Azerbaijan
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amerejea Tehran baada ya ziara rasmi ya siku moja mjini Baku ambako alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev.
Katika ziara hii, Rais wa Iran, pamoja na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev, walihudhuria na kutoa hotuba katika mkutano wa pamoja wa wanaharakati wa kiuchumi kutoka Iran na Azerbaijan, na pia kukutana na Wairani wanaoishi katika jiji la Baku.
Katika ziara hiyo, pamoja na taarifa ya pamoja kati ya marais wa Iran na Azerbaijan, hati saba za maelewano kuhusu ushirikiano pia zilitiwa saini kati ya maafisa wa nchi hizo mbili. Jumatatu, Aprili 28, Pezeshikian aliwasili Baku kwa mwaliko rasmi wa Rais wa Azerbajani Ilham Aliyev. Katika mkutano rasmi na maafisa wa Azerbaijan, Rais Pezeshkian alisisitiza kupanuliwa ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali.
Katika ziara hii ya siku moja, hati saba za maelewano kuhusu ushirikiano wa pamoja zilitiwa saini kati ya maafisa wa nchi hizo mbili, zikihusu masuala ya mashauriano ya kisiasa, uchukuzi, mabadilishano ya kitamaduni, ushirikiano wa afya, vyombo vya habari na uwekezaji. Aidha marais wa Iran na Azerbaijan walitia saini taarifa ya pamoja.
Katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Ilham Aliyev, Masoud Pezeshkian alisema: "Iran na Jamhuri ya Azerbaijan zinaweza kuanzisha amani na usalama katika eneo kwa msaada wa kila mmoja."

Daktari Pezeshkian pia alisema katika mkutano na wafanyabiashara wa Iran na Azerbaijan: "Tunaweza kuendeleza uhusiano kati ya Iran na Azerbaijan kama zamani." Lazima tuhamishe mafanikio ya kisayansi na kitamaduni na uzalishaji wa watu wa nchi hizi mbili kwa kila mmoja ili kuunda mazingira ya kila mmoja kunufaika.
Siasa za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinazozingatia diplomasia ya ujirani sio tu kwamba zinalenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kisiasa, bali pia zinalenga kuzidisha uhusiano wa kiutamaduni na kibinadamu kati ya mataifa ya eneo hili. Ziara rasmi ya Rais Pezeshkian huko Baku inachukuliwa kuwa hatua muhimu katika kupanuliwa uhusiano kati ya Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.
Safari hii iliyoambatana na ujumbe wa watu 120, inadhihirisha umakini wa Iran katika kutekeleza diplomasia hai na majirani zake.
Serikali ya awamu ya 14, kwa kutumia mbinu ya diplomasia ya ujirani, imechukua hatua madhubuti za kuboresha uhusiano na Jamhuri ya Azerbajani. Mbinu hii, ambayo inalenga kupunguza anga ya kutokuelewana na kuimarisha hali ya kuaminiana, imefungua njia ya ushirikiano endelevu katika maeneo muhimu kama vile utalii, mabadilishano ya kitamaduni, na miradi ya pamoja ya kuvuka mipaka.
Mtazamo huo chanya na wa kiutendaji wa siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeziweka nchi hizo mbili kwenye njia ya kuwa kigezo chenye mafanikio cha ushirikiano wa kieneo. Mtindo huu, uliojengwa juu ya kuheshimiana, kuongeza uwezo wa pamoja, na kuzingatia maslahi ya pande zote, unaweza kuimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya mataifa haya mawili na kujenga mustakabali mzuri kwa Tehran na Baku.
Matokeo ya kupanua ushirikiano na mazungumzo ya kisiasa yatakuwa ni kuunda na kujenga jukwaa la kuongeza mabadilishano ya kiuchumi kati ya Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.

Katika miaka ya hivi karibuni, huku mizozo na mivutano kuhusu eneo la Karabakh kati ya Jamhuri ya Azerbaijan na Armenia ikizidi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilichukua nafasi ipasavyo katika kusimamisha amani na utulivu katika eneo la Caucasus Kusini.
Suala jingine muhimu kwa Iran ni umuhimu wa uthabiti wa mipaka na uundaji wa njia za usafiri kwa kuzingatia kudumishwa usalama wa mipaka ya eneo la Caucasus kwa lengo la kupanua ushirikiano na majirani na, bila shaka, kupunguza ushawishi wa kigeni.
Safari ya Pezeshkian mjini Baku itaharakisha maendeleo ya uhusiano wa kiuchumi kati ya Iran na Jamhuri ya Azerbaijan. Mnamo 2024, biashara kati ya Jamhuri ya Azerbaijan na Iran ilifikia dola milioni 580, ikiwa ni ongezeko la 20% kabla ya mwaka uliopita. Hata hivyo, Baku na Tehran zinapanga kuongeza biashara ya kila mwaka ya nchi mbili hadi dola bilioni 10 ndani ya miaka mitano ijayo.
Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya uchumi, teknolojia na utamaduni pia utakuwa na matokeo chanya kwa nchi za eneo hilo. Iran na Jamhuri ya Azerbaijan zina uwezo wa kutosha katika sekta mbalimbali za kiuchumi, zikiwemo nishati, kupanua ushirikiano. Asili ya kihistoria ya uhusiano wa kitamaduni kati ya watu wa nchi hizo mbili pia itakuwa sababu nzuri ya kukuza ushirikiano katika nyanja mbalimbali.