Iran yaunga mkono 'mazungumzo ya jadi' na mataifa ya Ghuba ya Uajemi
-
Kamal Kharrazi
Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni la Iran amesisitiza haja ya kufanyika mazungumzo ya dhati na jadi kati ya Iran na nchi za Ghuba ya Uajemi, akiyaeleza mazungumzo hayo kama msingi wa utulivu katika eneo.
Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Ghuba ya Uajemi jana Alkhamisi, Kamal Kharrazi alisisitiza umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Iran na mataifa ya Kiarabu. Amesema serikali za kieneo zimepevuka na kuwa na mantiki, na kwamba Iran inaunga mkono kikamilifu majadiliano hayo.
Huku akisisitiza dhamira ya kimkakati ya Iran kwa diplomasia ya 'madaraka laini', Kharrazi amesema, "Sera hii inajumuisha kupanua ushirikiano wa kiuchumi na nchi jirani."
Ameonya dhidi ya njama za Israel za kulitawala eneo la Ghuba ya Uajemi, akisema Jamhuri ya Kiislamu na mataifa yanayopatikana katika eneo hili la kistratijia yanahitaji kufanya mazungumzo "mazito."
Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Iran amependekeza kuundwa muungano unaojumuisha Iran, Iraq na mataifa sita ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi, akisisitiza kuwa kwa pamoja yanaweza kufanya kazi ili kuimarisha usalama, maendeleo ya kiuchumi na ushirikiano wa kitamaduni katika eneo hili bila kuingiliwa na mataifa ya kigeni.
Zaidi ya ushirikiano wa kiuchumi, Kharrazi alisisitiza haja ya ushirikiano wa kina wa kikanda. "Ushirikiano katika nishati, sayansi na teknolojia, utamaduni, na urithi wa pamoja, pamoja na uratibu wa kisiasa na kijeshi, ni maeneo muhimu kwa maendeleo ya pamoja."
Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni la Iran ameongeza kuwa, "Mustakabali wa eneo hili unategemea kuimarishwa ushirikiano kati ya mataifa ya eneo, na Iran iko tayari kwa ushirikiano wa kina."