Araghchi: Iran iko tayari kwa mazungumzo ya 'kujenga', 'yasiyo na upendeleo' na Troika ya EU
(last modified Tue, 06 May 2025 06:40:40 GMT )
May 06, 2025 06:40 UTC
  • Araghchi: Iran iko tayari kwa mazungumzo ya 'kujenga', 'yasiyo na upendeleo' na Troika ya EU

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema Tehran iko tayari kufanya mazungumzo "ya kujenga na yasiyo na upendeleo" na nchi tatu zinazounda Troika ya Umoja wa Ulaya, ambazo ni Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu jana Jumatatu na mwakilishi mkuu wa EU kwa sera za mambo ya nje na usalama, Kaja Kallas, Araghchi amemfahamisha mwakilishi huyo wa Umoja wa Ulaya kuhusu matukio ya hivi punde kuhusu mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.
 
Amesema Iran iko tayari kuendeleza maingiliano na pande za Ulaya, ndani ya mfumo wa Umoja wa Ulaya na nchi tatu za Ulaya.
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza matumaini aliyonayo ya Iran na Troika ya Ulaya kuanza tena mazungumzo kwa kufuata muelekeo wa kujenga usiochochewa na chuki za kisiasa.
 
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu imechagua muelekeo wa uwajibikaji katika kutumia njia ya diplomasia kwa ajili ya kuushughulikia wasiwasi wa kubuni uliotengenezwa kuhusiana na mpango wake wa amani wa nyuklia, na akatilia mkazo haja ya kufuata njia hiyo kwa kuonyesha dhamira ya dhati na kuzingatia uhalisia.
 
Araghchi amefafanua kuwa, ikiwa dai la uwezekano wa Iran kupata silaha za nyuklia linatokana na wasiwasi tu zilionao pande zingine katika mazungumzo, wasiwasi huo unaweza kupunguzwa; na akaongezea kwa kusema: "inawezekana kikamilifu kufikia makubaliano katika suala hili, lakini kuna haja ya kujiepusha na misimamo isiyoendana na uhalisia na isiyo na mantiki".

Kwa uratibu wa Oman, Iran na Marekani zimefanya duru tatu za mazungumzo katika mji mkuu wa Oman Muscat na mji mkuu wa Italia wa Roma mnamo Aprili 12, 19, na 26 kwa lengo la kufikia makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran mkabala wa kuondolewa vikwazo ilivyowekewa Tehran.../