Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudi Arabia wakutana Jeddah
(last modified Sun, 11 May 2025 04:18:55 GMT )
May 11, 2025 04:18 UTC
  • Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudi Arabia wakutana Jeddah

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudi Arabia wamekutana kujadili masuala muhimu yanayohusu uhusiano wa pande mbili, pamoja na matukio ya kikanda na kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alikutana na mwenzake wa Saudi Arabia, Prince Faisal bin Farhan Al Saud, jijini Jeddah, jana Jumamosi.

Ziara ya Araghchi nchini Saudi Arabia ni sehemu ya sera inayoendelea ya Tehran ya kuimarisha uhusiano na nchi jirani.

Ijumaa, Araghchi alitangaza kuwa duru ya nne ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani itafanyika Oman leo Jumapili.

Akizungumza katika mahojiano siku ya Ijumaa, Araghchi alisema ziara yake Saudi Arabia inakwenda sambamba na mashauriano kati ya nchi hizo mbili kuhusu masuala ya kikanda na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.

Aliongeza kuwa tangu kuanza kwa mazungumzo hayo Aprili mwaka huu, Iran imekuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara na nchi za eneo hilo ili kuwapa taarifa kuhusu mchakato huo.

Kwa upatanishi wa Oman, Iran na Marekani zimefanya duru tatu za mazungumzo katika mji mkuu wa Oman, Muscat, na mji mkuu wa Italia, Rome, mnamo Aprili 12, 19 na 26, zikilenga kufikia makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na kuondoa vikwazo dhidi ya Tehran.

Pande zote mbili hadi sasa zimeelezea kuridhishwa na jinsi mazungumzo yanavyoendelea, zikiyataja kuwa ni “chanya” na “yanayoendelea vizuri.”

Duru ya nne ya mazungumzo hayo ilikuwa imepangwa kufanyika Mei 3 huko Muscat lakini ikaahirishwa kwa “sababu za kiufundi,” kama alivyonukuliwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.