Pezeshkian: Iran inaunga mkono usitishaji vita baina ya India-Pakistan
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono usitishaji vita wa kudumu kati ya India na Pakistan, akitoa mwito wa kufanyika mazungumzo kati ya nchi za kikanda ili kutatua mizozo iliyopo na kuimarisha amani.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif hapa Tehran jana Jumatatu, Pezeshkian amesisitiza umuhimu wa mashauriano zaidi kati ya nchi za kikanda na washirika wengine wa kimataifa ili kufikia lengo hilo.
Kadhalika Dakta Pezeshkian amesema mpaka kati ya Iran na Pakistan lazima ulindwe dhidi ya aina yoyote ya ukosefu wa usalama na ugaidi.
Amesisitiza kuwa, hivi sasa Asia Magharibi na Asia Kusini zinahitaji usalama na amani zaidi kuliko wakati mwingine ule, jambo ambalo linasisitiza haja ya mashauriano na maingiliano chanya na nchi jirani na washirika wengine wa kimataifa.
Pezeshkian amesema kuwa, yeye na Waziri Mkuu wa Pakistan pia wamejadili masuala ya kikanda na ulimwengu wa Kiislamu, ikiwa ni pamoja na ukatili unaoendelea wa Israel huko Gaza.
Amesema Iran na Pakistan zikiwa wanachama wawili wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na watetezi wa kadhia ya Palestina, zinalaani jinai hizo na uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa utawala wa Israel.
Rais wa Iran ameongeza kuwa, "Tehran na Islamabad zimetoa wito kwa nchi za Kiislamu kuwaunga mkono kikamilifu watu wanaodhulumiwa wa Palestina na Gaza."
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif kwa upande wake, amesema nchi yake inaunga mkono kwa uthabiti mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, akisisitiza kwamba Pakistan haitaruhusu mtu yeyote kutumia vibaya eneo lake kutekeleza hatua za kichokozi dhidi ya Iran.