Malengo halisi ya Magharibi kuhusu Iran ni yapi?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128938
Vyombo vya habari vya kigeni, sambamba na kuripoti kauli ya hivi karibuni ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, vimezingatia kwa namna ya kipekee sehemu ya hotuba yake ambapo amesisitiza kuwa: “Mpango wa nyuklia, urutubishaji na haki za binadamu ni visingizio – wanachotaka wao ni dini na elimu yenu.”
(last modified 2025-07-30T11:59:23+00:00 )
Jul 30, 2025 11:59 UTC
  • Malengo halisi ya Magharibi kuhusu Iran ni yapi?

Vyombo vya habari vya kigeni, sambamba na kuripoti kauli ya hivi karibuni ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, vimezingatia kwa namna ya kipekee sehemu ya hotuba yake ambapo amesisitiza kuwa: “Mpango wa nyuklia, urutubishaji na haki za binadamu ni visingizio – wanachotaka wao ni dini na elimu yenu.”

Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jumanne tarehe 29 Julai, katika hafla ya kumbukumbu ya mashujaa wa vita vya siku 12 vya kulazimishwa vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, alisisitiza kuwa Iran ya Kiislamu imejengwa kwa msingi wa “dini” na “elimu”. Katika ujenzi wa Jamhuri ya Kiislamu, vipengele viwili vya “dini” na “elimu” ni vipengele vikuu. Hivyo basi, dini ya wananchi na elimu ya vijana wetu imeweza kuwalazimisha maadui kurudi nyuma katika nyanja nyingi tofauti. Na hali hii itaendelea vivyo hivyo baada ya hapa.

Katika kuelezea sababu halisi za uadui wa Magharibi dhidi ya Iran, amesema: 'Kile ambacho mabeberu wa kimataifa, wakiongozwa na Marekani dhalimu, wanakipinga, ni dini yenu na elimu yenu; wanapinga dini yenu, wanapinga imani hii pana ya watu, wanapinga umoja huu chini ya kivuli cha Uislamu na Qur'ani; na wanapinga elimu yenu. Kwamba baada ya ushindi wa Mapinduzi hadi leo, idadi ya watu wa Iran imeongezeka mara mbili, lakini idadi ya wanafunzi huenda imeongezeka mara kumi au zaidi , jambo hili linawaudhi; kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaweza kuleta ubunifu katika nyanja mbalimbali za elimu, iwe ni elimu ya kibinadamu, ya kiufundi au ya kidini,  linawaudhi; wanalipinga hili. Yale wanayosema kuhusu suala la nyuklia, urutubishaji na haki za binadamu na mengineyo ni visingizio tu; kiini cha suala hili kiko hapo.'

Matamshi ya karibuni ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena yanaonyesha asili ya uadui wa Magharibi, hasa Marekani, sambamba na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Marekani na washirika wake wa Magharibi mara nyingi wameituhumu Iran na kuihusisha na masuala kama vile uwezo wa nyuklia hasa urutubishaji wa urani, pamoja na kuihusisha na ukiukaji wa haki za binadamu na pia kuihusisha na kuunga mkono ugaidi, hasa katika eneo la Asia Magharibi.

Mbali na ukweli kwamba Wamagharibi hutumia undumakuwili katika kuamiliana na mataifa na serikali mbalimbali, lakini ukweli kwamba hubuni mara kwa mara visingizio na kutafuta visingizio vya kuiwekea Iran mashinikizo hadi kufikia kuishambulia kijeshi, unaonyesha kuwa Marekani na washirika wake kama vile troika ya Ulaya pamoja na utawala wa Kizayuni kimsingi wana tatizo na asili ya Jamhuri ya Kiislamu na hawawezi kuvumilia uhai wake.

Jambo la kuvutia ni kwamba matamshi muhimu sana na ya msingi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kufafanua sababu halisi za uadui wa Magharibi dhidi ya Iran yamevutia pia vituo vya tafiti vya Magharibi. Kituo cha Foundation for Defense of Democracies, kilicho karibu na Bunge la Marekani, katika uchambuzi wa matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kimeandika: 'Ayatullah Khamenei ameishutumu Magharibi kwa kutumia suala la nyuklia kama kisingizio cha kudhoofisha Jamhuri ya Kiislamu. Tovuti ya Foundation for Defense of Democracies imeeleza kuwa matamshi ya Kiongozi Muadhamu yanaonyesha kuwa Iran haina nia ya kusitisha urutubishaji na imeazimia kuendelea kuunga mkono mhimili wa mapambano katika eneo hilo na wakati huo huo, kujenga upya mpango wake wa nyuklia na makombora. Kituo hiki kimeeleza kuwa matamshi ya karibuni ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu yanaonyesha kuwa vita vya kulazimishwa vya siku 12 havikuathiri mwelekeo wa Jamhuri ya Kiislamu katika nyanja zote za nyuklia na kikanda.

Iran katika kipindi cha miongo minne baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu imeweza kupiga hatua kubwa katika kujitegemea na kukuza uwezo wa ndani na kupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi kwa mataifa ya nje katika nyanja za kimkakati kama vile sekta ya mafuta na gesi, petrokemikali, viwanda vikubwa na maeneo mengine ya viwanda. Kwa upande mwingine, wanasayansi na watafiti vijana wa Iran wameweza kupata mafanikio makubwa katika teknolojia za hali ya juu kama vile teknolojia ya nano, seli shina na sekta ya anga za juu. Iran pia imeweza kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya elimu na taasisi za elimu ya juu.

Kuimarika kwa kiwango cha kielimu cha jamii, ongezeko la kiwango cha usomaji na uandishi, ongezeko la vituo vya elimu ya shule na vyuo vikuu, ongezeko la idadi ya wanafunzi katika fani mbalimbali, nafasi ya juu ya Iran katika idadi ya machapisho na marejeo ya kisayansi, usajili wa uvumbuzi na ubora katika teknolojia za nano, nyuklia, anga za juu na seli shina, ni baadhi ya mafanikio makuu ya kisayansi na kiteknolojia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Pia ongezeko kubwa la idadi ya vyuo vikuu linaweza kuchukuliwa kama mojawapo ya vigezo vya maendeleo ya elimu ya juu nchini Iran. Idadi ya vyuo vikuu nchini Iran ambayo kabla ya mapinduzi ilikuwa takriban matawi 15 ya vyuo vikuu, leo imefikia zaidi matawi  2,640. Ukuaji wa idadi ya wanafunzi ni kiashiria kingine cha maendeleo ya elimu baada ya Mapinduzi ya Kiislamu. Wakati ambapo idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu kabla ya Mapinduzi haikuzidi 155,000, leo zaidi ya wanafunzi milioni 4.2 wanasoma nchini Iran. Wakati huo huo, Magharibi ina hofu kwamba Iran ya Kiislamu, kama jamii ya kidini ambayo imepata maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali, itapata kutambuliwa duniani.

Maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kwa namna ambayo hata maadui wameyakiri na hawawezi kuyakana. Mafanikio ya kisayansi na kufikiwa kwa teknolojia mpya na za kisasa yamewashangaza hata Wamagharibi, hasa Marekani, na kuibua wasiwasi mkubwa ambao umesababisha kuongezeka kwa mashinikizo, hujuma, vikwazo na hivi karibuni, kuanzishwa kwa vita vya kulazimishwa kwa visingizio kama vile suala la nyuklia. Kwa hakika, maadui wa Iran ya Kiislamu wana hofu kubwa kutokana na maendeleo ya haraka na ongezeko la uwezo wa Iran ikiwa ni pamoja na kiuchumi na kibiashara, kisayansi na kiufundi, kijamii na kiutamaduni pamoja na siasa zake za nje zinazobadilika na uwezo wake wa kijeshi wa kuzuia mashambulizi – na haya yote ndicho chanzo cha uhasama wao unaozidi kuongezeka kila siku dhidi ya Iran.