Pezeshkian: Migawanyiko kati ya mataifa ya Kiislamu inainufaisha Israel pekee
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129984-pezeshkian_migawanyiko_kati_ya_mataifa_ya_kiislamu_inainufaisha_israel_pekee
Rais wa Iran amesema umoja wa wananchi wa Iran na katika mataifa yote ya Kiislamu ndiyo kinga kuu dhidi ya vitisho vya maadui, akionya kuwa migawanyiko ni kwa maslahi ya Israel pekee.
(last modified 2025-08-25T11:00:48+00:00 )
Aug 25, 2025 11:00 UTC
  • Pezeshkian: Migawanyiko kati ya mataifa ya Kiislamu inainufaisha Israel pekee

Rais wa Iran amesema umoja wa wananchi wa Iran na katika mataifa yote ya Kiislamu ndiyo kinga kuu dhidi ya vitisho vya maadui, akionya kuwa migawanyiko ni kwa maslahi ya Israel pekee.

Rais Masoud Pezeshkian amesema jambo muhimu zaidi linaloweza kuilinda nchi dhidi ya vitisho na mashambulizi ya maadui ni mshikamano wa kitaifa na kikanda. Amesisitiza kuwa, "Kuibua mgawanyiko ndani ya nchi au miongoni mwa mataifa ya Kiislamu, ni sawa na kuitumikia Israel."

Rais wa Iran ameyasema hayo mapema leo Jumatatu alipotembelea Haram ya Muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Imam Rouhollah Khomeini (MA).

Amesisitiza kuwa, Israel na Marekani zinataka kuwagonganisha Wairani na kuwafanya Waislamu wa eneo hili wawe kwenye mizozo na mivutano isiyoisha. "Lazima tukubaliane kwamba, hatupasi kugawanyika.  Hatufai kuwa na uadui au uhasama tunapoamiliana na majirani zetu. Ni ndugu zetu," amesema.

Dakta Pezeshkian ameeleza bayana kuwa, "Nchi zote jirani ni ndugu, majirani, na jamaa zetu. Migawanyiko na utengano huu ulianzishwa na mabeberu na watafuta madaraka. Waislamu lazima waungane dhidi ya adui. Jaribio lolote la kutugawanya nyumbani au miongoni mwa Waislamu ni huduma kwa Israel."

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, "Tukiwa wamoja adui hatathubutu kuwatazama Waislamu kwa dharau, ni lazima tujitahidi kwa pamoja, tuonyeshe kwa vitendo kwamba tumejitolea kuwatumikia wananchi na kamwe tusilegee katika kushughulikia matatizo yao, nyumbani na kwa majirani zetu Waislamu, tutafanya kazi ya kuimarisha umoja na mshikamano siku baada ya siku."

Rais na wajumbe wake wa Baraza la Mawaziri wamefanya ziara katika Haram Tukufu iliyoko kusini mwa mji mkuu Tehran, ili kujadidisha utiifu wao kwa itikadi za Imam Khomeini MA. Wamefanya hivyo kwa mnasaba wa Wiki ya Utawala iliyoanza Jumapili.