Kwa nini Iran inataka hatua kali zaidi zichukuliwe na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu dhidi ya utawala wa Kizayuni?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130054-kwa_nini_iran_inataka_hatua_kali_zaidi_zichukuliwe_na_jumuiya_ya_ushirikiano_wa_kiislamu_dhidi_ya_utawala_wa_kizayuni
Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran karibuni hivi alifika mjini Jeddah, Saudia kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na kukitaja kikao hicho kuwa mtihani wa kihistoria kwa Umma wa Kiislamu na pengine miongoni mwa fursa chache za kuunda muungano wa kieneo na kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2025-08-27T07:14:03+00:00 )
Aug 27, 2025 07:14 UTC
  • Kwa nini Iran inataka hatua kali zaidi zichukuliwe na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu dhidi ya utawala wa Kizayuni?

Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran karibuni hivi alifika mjini Jeddah, Saudia kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na kukitaja kikao hicho kuwa mtihani wa kihistoria kwa Umma wa Kiislamu na pengine miongoni mwa fursa chache za kuunda muungano wa kieneo na kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Abbas Araghchi aliwasili Jeddah Jumapili Agosti 24 akiongoza ujumbe wa kidiplomasia kwa ajili ya kushiriki kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC. Madhumuni ya kikao hicho yalitangazwa kuwa ni kuchunguza maafa ya kibinadamu huko Gaza, kuratibu utoaji wa misaada ya dharura na pia kuchunguza pande za kisheria na kisiasa za uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kuikalia kwa mabavu Gaza.

Katika mkesha wa kikao hicho, Araghchi aliandika makala katika gazeti la Sharq Al-Awsat chini ya anwani "Ndoto ya Israel Kubwa ni hatari na tishio kwa amani na usalama wa kimataifa" kwamba: "Kikao kijacho cha mawaziri wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kilipaswa kuwa hatua ya mabadiliko yanayounganisha pamoja azma ya nchi za Kiislamu ya kuzuia tamaa isiyo na kikomo ya Netanyahu na genge lake la mawaziri waziri wenye misimamo ya kufurutu ada, kwa ajili ya kuzuia kuendelea mauaji ya watu wasio na hatia, uharibifu wa nchi za Kiislamu na unyakuzi wa ardhi zao."

Araghchi alisema kikao hicho hakikupasa kutangaza kwa maneno tu mshikamano wake na taifa la Palestina au kueleza masikitiko na wasiwasi wake juu ya hali ya sasa, bali ilikuwa fursa ya kihistoria kwa Umma wa Kiislamu kuunda muungano wa kieneo na kimataifa ili kusimamisha uchokozi na uvamizi wa Israel.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alisisitiza zaidi kuwa, kikao hicho kilipasa kutoa mashinikizo makubwa zaidi ya kisiasa na kidiplomasia kupitia kuundwa muungano wenye nguvu wa kimataifa utakaoulazimisha utawala wa Kizayuni kusimamisha mara moja mauaji ya kimbari na kufuta miradi yake ya kupenda kujitanua, kupora na kukalia kwa mabavu ardhi za Waislamu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa wananchi wa Palestina kwa kuzingatia misingi ya kibinadamu na kimaadili na imekuwa ikitetea haki halali za Wapalestina katika uga wa kimataifa kupitia msururu wa hatua za kisiasa na kidiplomasia.

Safari ya Araghchi mjini Jeddah 

Iran bila shaka ni mtetezi wa haki za Wapalestina na inachukulia hatua za jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu. Kwa mtazamo huu, kimya au hatua dhaifu za nchi za Kiislamu zinachukuliwa kuwa hazitoshi na suala lisilokubalika kabisa. Kuhusiana na hili, inasikitisha kuona kwamba baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu zimeanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni. Iran inauchukulia mchakato huu kuwa usaliti kwa kadhia ya Palestina hivyo inataka kuona msimamo wa wazi na wa umoja ukichukuliwa dhidi ya siasa hizo mbovu na zenye madhara kwa taifa la Palestina.

Kufuatia mashambulizi ya jinai ya mara kwa mara huko Gaza, Msikiti wa Al-Aqsa na maeneo ya makazi ya Wapalestina, Iran inataka kuona jibu la kivitendo likitolewa na sio kauli za kulaani tu za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu. Ikiwa na nchi wanachama zaidi ya 50, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ina uwezo mkubwa wa kutoa mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya utawala wa Kizayuni, uwezo ambao Iran inataka utumike vizuri kwa maslahi ya umma wa Kiislamu.

Jumuiya hii inaweza kuongeza mashinikizo ya kieneo na kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa kutekeleza hatua kadhaa za kisiasa, kiuchumi na kisheria. Iran imependekeza nchi za Kiislamu ziunde muungano thabiti dhidi ya siasa za kupenda kujitanua za utawala wa Kizayuni. Muungano huu unaweza kuwa na sauti ya pamoja katika vikao vya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa na kutaka vikwazo au hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watawala katili wa Israel.

Nchi za Kiislamu bila shaka zinaweza kukata au kupunguza kwa kiasi kikubwa uhusiano wa kiuchumi na utawala wa Kizayuni. Hii ni pamoja na kupiga marufuku uagizaji wa bidhaa zinazozalishwa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, kukata ushirikiano wa kiteknolojia na kusimamisha uwekezaji wa pamoja na utawala huo. Kufuatilia jinai za kivita na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na viongozi wa utawala wa Kizayuni katika mahakama za kimataifa kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kunaweza kutoa mashinikizo makubwa ya kisheria na ya vyombo vya habari dhidi ya utawala huo ghasibu.

Kwa upande mwingine, kutuma misaada ya kibinadamu, kusaidia taasisi za kiraia za Palestina na kuimarisha vyombo huru vya habari kunaweza kuimarisha muqawama wa ndani. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu inaweza kuanzisha kampeni kubwa za vyombo vya habari ili kufichua jinai za utawala wa Kizayuni na kuhamasisha maoni ya umma ya ulimwengu dhidi ya watendajinai wa Israel.

Kama kikao cha Jeddah kingeweza kutekeleza vizuri matakwa ya Umma wa Kiislamu, ikiwa ni pamoja na kutoa jibu lililoratibiwa, kingeweza kudhihirisha umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu na hivyo kukabiliana vilivyo na jinai za utawala wa Kizayuni, katika hali ambayo Marekani na serikali za Magharibi daima ni waungaji mkono na washiriki wakuu wa jinai zinazofanywa na watawala wa Tel Aviv dhidi ya Waislamu wasio na hatia.