Mbunge wa Hizbullah: Kukubali tupokonywe silaha ni sawa na kujinyonga
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129330
Mbunge wa Lebanon kutoka mrengo wa kisiasa wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya nchi hiyo Hizbullah amelipinga vikali dai la kuitaka harakati hiyo iweke chini silaha zake kufuatia shinikizo la Marekani kwa serikali la kuitaka iipokonye silaha harakati hiyo.
(last modified 2025-08-09T07:22:42+00:00 )
Aug 09, 2025 07:22 UTC
  • Mbunge wa Hizbullah: Kukubali tupokonywe silaha ni sawa na kujinyonga

Mbunge wa Lebanon kutoka mrengo wa kisiasa wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya nchi hiyo Hizbullah amelipinga vikali dai la kuitaka harakati hiyo iweke chini silaha zake kufuatia shinikizo la Marekani kwa serikali la kuitaka iipokonye silaha harakati hiyo.

Kiongozi wa mrengo wa Muungano wa Uaminifu kwa Muqawama, Mohammad Raad ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya al-Manar baada ya Waziri Mkuu wa Lebanon Nawaf Salam kutangaza kuwa mawaziri wameidhinisha "malengo" ya pendekezo lililotolewa na Marekani.

"Kukubali kupokonywa silaha ni kujinyonga, na hatuna nia ya kujinyonga," ameeleza mbunge huyo akisisitiza kuwa kukubali kuweka chini silaha ni sawa na kulisaliti taifa.

Raad amebainisha wazi kwamba kuweka chini silaha si chaguo tu la kisiasa, bali ni mstari mwekundu unaohusiana na suala la kuendelea kuwepo au kutoweka.

"Kusema salimisha silaha zako ni kusema salimisha heshima yako ... Nani atadhamini mamlaka kamili ya kujitawala ikiwa silaha zitasalimishwa?" amehoji mbunge huyo wa Hizbullah.

Raad ametoa indhari pia kwa kusema, wapitishaji maamuzi ya kisiasa juu ya suala la kutaka Hizbullah ipokonywe silaha watawajibika na kubeba dhima ya athari zote za maamuzi watakayochukua.

Wakati huohuo, harakati yenyewe ya Hizbullah imesisitiza kwamba inayachukulia maamuzi ya serikali kama kwamba ni kitu ambacho hakipo.../