Norway yasimamisha uwekezaji katika makampuni 11 ya Israel
Hazina ya Utajiri wa Taifa wa Norway imetangaza kuwa imesitisha uwekezaji katika makampuni 11 ya utawala wa Israel ambayo yamewekeza katika kampuni ya utengenezaji wa injini za ndege.
Nikolay Tangen, mkuu wa Benki ya Usimamizi wa Uwekezaji ya Norway, ambayo inasimamia hazina ya utajiri wa nchi hiyo, alisema Jumatatu kwamba Uamuzi huo umechukuliwa kujibu "hali isiyo ya kawaida," inayoendelea huko Gaza.
Tangen amesema: 'Hali ya Gaza ni maafa makubwa ya kibinadamu. Tuliwekeza katika makampuni yanayofanya kazi katika nchi yenye vita, na hali katika Ukingo wa Magharibi na Gaza imekuwa mbaya zaidi.'
Hazina ya Utajiri wa Taifa ya Norway, pia inayojulikana kama hazina ya mafuta, ambayo huhifadhi mapato ya nishati ya nchi hiyo, ina thamani ya dola trilioni 1.9 na ndiyo kubwa zaidi ya aina yake. Hazina hiyo imewekeza katika zaidi ya makampuni 8,600 duniani
Gazeti la Norway la "Aftenposten" liliripoti wiki iliyopita kwamba hazina hiyo imewekeza katika kampuni ya Kizayuni ya "Bet Shamsh", ambayo inazalisha sehemu za injini za ndege za kivita zinazotumiwa na wanajeshi wa Israel.
Kufuatia ufichuzi huu, Jonas Gaher Store Waziri Mkuu wa Norway alimwomba Waziri wa Fedha Jens Stoltenberg kutazama upya uwekezaji katika makampuni ya aina hiyo.
Stoltenberg Jumatatu alisifu uamuzi huo wa Benki ya Uwekezaji ya Norway kwa kuchukua "hatua ya haraka" katika uwanja huo.
Waziri mkuu wa Norway amesema kwamba kanuni za kimaadili za hazina hiyo zinasema kwamba isiwekeze katika makampuni ambayo yanasaidia kukiukwa sheria za kimataifa.
Stoltenberg amesisitiza kuwa hazina hiyo haupaswi kuwa na hisa katika "makampuni yanayounga mkono vita vya Israel dhidi ya Gaza au kukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi."