Imekuwaje Muungano wa Nchi za Magharibi na Marekani Sasa Unaelekea Kutoweka?
Jarida la Foreign Policy la nchini Marekani limetahadharisha kuwa, vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Iran ni nukta ya kushuhudiwa mabadiliko muhimu yanayopelekea kudhoofika muungano wa Magharibi.
Ikilinukuu shirika la habari la ISNA, tovuti ya Pars Today imeripoti kuwa, jarida la Foreign Policy limeandika katika uchambuzi wake: Vita dhidi ya Iran si mzozo wa kieneo tu, bali ni nukta ya mabadiliko muhimu ya kijiopolitiki ambayo yamesambaratisha kwa kishindo kikubwa mfumo wa kimataifa uliohodhiwa na kudhibitiwa na Marekani.
Uchambuzi huo unasisitiza kuwa, vita ilivyolazimishwa kupigana Iran "vimetoa kipigo angamizi kwa mfumo wa kimataifa unaokaribia kukata roho ulioko chini ya uongozi wa Marekani" na kwamba Washington sasa imegeuka kuwa "tishio kubwa zaidi kwa mfumo wa kimataifa." Jarida hilo linalochapishwa nchini Marekani limeendelea kueleza kwamba, hatua ya rais wa nchi hiyo Donald Trump ya kutangulia kuanzisha vita vivi hivi tu pasi na kuwa na hoja na mashiko ya kisheria “imeurasimisha uvamizi na uchokozi kuwa mbinu na njia ya kawaida ya kutatua tofauti baina ya nchi mbalimbali”.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa jarida la Foreign Policy, kwa kauli yake Trump ya kutishia kuteketeza miundombinu ya kiraia na hata kuangamiza ustaarabu mzima, "ameugeuza uhalifu wa kivita kuwa taktiki ya kijeshi na turufu ya kurubuni kidiplomasia kwenye meza ya mazungumzo." Kitendo cha jeshi la wanamaji la Marekani cha kuweka zuio la baharini katika Mlango-Bahari wa Hormuz nacho pia kimeelezewa kuwa ni “kulifanya jambo la kawaida suala la kuizingira kwa silaha njia ya kijiografia ya uchumi wa dunia", jambo ambalo limeutia doa kubwa uaminifu na itibari ya kimaadili na kisheria ya Marekani.

Jarida la Foreign Policy limeendelea kueleza katika uchambuzi wake kwamba, vita dhidi ya Iran sio tu vimesambaratisha mfumo wa wa kimataifa, lakini pia vimedhoofisha muungano wa nchi za Magharibi wanachama wa mkataba wa kijeshi wa pande mbili za Atlantiki, NATO. Nchi za Ulaya zimekataa kutekeleza ombi na wito wa Trump wa kuzitaka zipeleke vikosi vyao vya wanamaji kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz na zimeweka mpaka pia wa kutumiwa kambi zao kwa ajili ya kuishambulia kijeshi Iran. Katika mjibizo aliotoa kwa hatua hizo, Trump amewaita washirika wa Marekani wa barani Ulaya "waoga" na kutishia kujitoa kikamilifu katika shirika la kijeshi la NATO.
Uchambuzi wa Foreign Policy unamalizia kwa kusisitiza kwamba: "Vita hivi vinaweza kuingia na kusajiliwa katika historia kama hati rasmi ya kutengana Washington na washirika wake wa Ulaya" na kuharakisha hatua ya Ulaya kuelekea kwenye mkakati wa kujitosheleza na kujitegemea kiulinzi na hata kinyuklia…/