Vijana wa Kisomali wachukua udhibiti wa meli ya mafuta
Taarifa zinasema meli ya mafuta iliyokuwa imebeba mapipa 18,500 ya mafuta na wafanyakazi 17 katika pwani ya kaskazini mashariki Somalia imechukuliwa na vijana wa Kisomali.
Taarifa za awali zinaashiria kuwa vijana waliokuwa na silaha walichukua udhibiti meli ya mafuta iitwayo “Honor 25” katika Ghuba ya Aden, karibu na Lango Bahari la Bab al-Mandab kwenye pwani ya Somalia siku ya Jumanne. Kundi la wahudumu wa meli hiyo linajumuisha nahodha ambaye ni raia wa Indonesia na pia Wapakistani 11.
Kwa sasa, meli hiyo imetiwa nanga karibu na pwani kati ya vijiji vya uvuvi vya Xaafun na Bander Beyla, kwa mujibu wa maafisa.
Mamlaka zinaamini kuwa washambuliaji walianzisha operesheni hiyo kutoka eneo la pwani lisilo na makazi makubwa karibu na Bander Beyla.
Serikali ya Shirikisho la Somalia, sambamba na majeshi ya majini ya kimataifa yanayolinda doria katika eneo hilo, bado hawajatoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo.
Hayo yanajiri siku chache baada ya Somalia kutangaza kupiga marufuku meli za utawala wa Israel kupita katika Lango Bahari la Bab al‑Mandab kama jibu kwa hatua ya utawala huo ya kulitambua rasmi eneo lililotangaza kujitenga na Somalia la “Somaliland”.
“Abdullahi Warfa”, balozi wa Somalia huko Ethiopia na pia katika Umoja wa Afrika, akijibu hatua ua utawala wa kizayuni wa Israel ya kutambua rasmi kujitenga eneo la Somaliland, ameonya kwamba aina yoyote ya kuingilia mamlaka ya Mogadishu itasababisha madhara makubwa.
Warfa ameongeza kuwa nchi yoyote itakayoingilia masuala ya ndani ya Somalia na kuathiri ukamilifu wa ardhi na mamlaka yake itakabiliana na matokeo mabaya, yakiwemo vizuizi vya kupita katika mlango‑bahari wa Bab al‑Mandab.