Maandamano makubwa nchini Tunisia na Morocco kupinga vita na kuzingirwa Gaza
Mamia ya Waafrika kaskazini mwa Afrika kwa mara nyingine tena wamejitokeza mitaani kuelezea upinzani wao dhidi ya vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza na siasa za kuwalazimishia njaa wakazi wa ukanda huo.
Shirika la habari la Sputnik limeripoti kwamba Jumatatu usiku, mamia ya raia wa Tunisia walikusanyika mbele ya Jumba la Michezo la Tunis lililoko kwenye Mtaa wa Habib Bourguiba. Mkusanyiko huo ulifanyika kwa mwaliko wa harakati ya "Uratibu wa Hatua za Pamoja kwa Palestina" ambapo waandamanaji walipiga nara za kukomeshwa mara moja vita na jinai dhidi ya watu wa Gaza.
Washiriki walielezea shambulio la hivi karibuni la jeshi la Israel dhidi ya timu ya habari ya Al Jazeera huko Gaza kama "uhalifu uliopangwa kwa makusudi wa kunyamazisha sauti ya ukweli na kuficha uhalifu wa zaidi ya miezi 22 dhidi ya watu waliozingirwa."
Waandamanaji walionya kuwa kulengwa kwa waandishi wa habari ni sehemu ya juhudi za kuweka udhibiti wa vyombo vya habari na kuweka msingi wa kufanya uhalifu mkubwa zaidi katika siku sijazo.
Nchini Morocco, kundi la wananchi limelaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Gaza kwa kufanya mikusanyiko na maandamano kama hayo.