Wakuu wa Majeshi ya Iran na Afrika Kusini Wafanya Mazungumzo mjini Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129458
Jenerali Rudzani Maphwanya, Kamanda wa Jeshi la Ulinzi wa Kitaifa la Afrika Kusini, amekutana mjini Tehran na Meja Jenerali Amir Hatami, Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo wamesisitiza uhusiano wao mkubwa wa kupambana na ukoloni na uungaji mkono wa pamoja kwa watu wanaodhulumiwa wa Gaza.
(last modified 2025-08-12T14:00:33+00:00 )
Aug 12, 2025 14:00 UTC
  • Wakuu wa Majeshi ya Iran na Afrika Kusini Wafanya Mazungumzo mjini Tehran

Jenerali Rudzani Maphwanya, Kamanda wa Jeshi la Ulinzi wa Kitaifa la Afrika Kusini, amekutana mjini Tehran na Meja Jenerali Amir Hatami, Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo wamesisitiza uhusiano wao mkubwa wa kupambana na ukoloni na uungaji mkono wa pamoja kwa watu wanaodhulumiwa wa Gaza.

Mkutano huo umeangazia kuimarika kwa ushirikiano wa kijeshi na kisiasa kati ya Iran na Afrika Kusini, wahusika wawili wenye ushawishi mkubwa na wanaopinga utawala wa mabavu wa nchi za Magharibi. Msimamo wao wa umoja unaashiria mabadiliko yanayoweza kutokea katika ushirikiano wa kimataifa na kuimarishwa uungaji mkono kwa Wapalestina katika wakati huu mgumu.

Iran na Afrika Kusini zina historia ndefu ya mshikamano dhidi ya ubeberu na zinalaani vikali jinai za Israel huko Gaza. Hatua ya hivi karibuni ya kisheria ya Afrika Kusini dhidi ya utawala haramu wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ na uungaji mkono wa Iran kwa Gaza zinathibitisha muungano wao unaoendelea kuimarika na uliokita mizizi katika kupigania haki, haki za binadamu na muqawama dhidi ya ushawishi wa Magharibi.

Meja Jenerali Hatami amepongeza msimamo wa kijasiri wa Afrika Kusini dhidi ya uvamizi wa Israel na kutoa wito wa kuungwa mkono kivitendo watu wanaodhulumiwa huko Gaza.

Jenerali Maphwanya amelaani mashambulizi ya Israel dhidi ya raia na waandishi wa habari na kusisitiza dhamira ya Afrika Kusini ya kuimarisha uhusiano wake wa kiulinzi na Iran, akiielezea ziara hiyo kuwa ni ujumbe wa kisiasa wa mshikamano.