Je, nini hatima ya kuipokonya silaha Hizbullah ya Lebanon?
Katika wiki za hivi karibuni, mpango wa kuipokonya silaha Hizbullah nchini Lebanon umewasilishwa kwa mashinikizo ya Marekani na uungaji mkono wa utawala ghasibu wa Israel.
Mpango wa kuipokonya silaha Hizbullah umeibua hali ya joto katika anga ya kisiasa ya nchi hiyo kiasi kwamba imezua wasiwasi mkubwa katika eneo zima la Asia Magharibi. Mpango huu ambao ulimependekezwa na Marekani na kuungwa mkono kikamilifu na Israel na baadhi ya serikali vibaraka za eneo, kwa mtazamo wa wachunguzi wengi, sio tu kwamba ni ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala Lebanon, bali pia, kwa kupuuza hali halisi ya kisiasa na kiusalama ya nchi hiyo, unaleta hatari ya kukosekana utulivu wa ndani na kuongezeka mivutano ya kieneo.
Hizbullah ilibuniwa katika miaka ya 1980 kwa ajili ya kupambana na uvamizi wa Israel na imekuwa nguvu kubwa yenye majukumu ya kijeshi, kisiasa na kijamii. Ushindi wake katika ukombozi wa kusini mwa Lebanon (2000) na Vita vya Siku 33 (2006) umeifanya kuwa nembo ya mapambano ya kitaifa. Mkataba wa Taif (1989) pia ulitambua rasmi silaha za Hizbullah kama chombo cha mapambano. Wakati huo huo, Azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama (2006) na usitishaji vita wa Novemba 2024 ulisisitiza upokonyaji silaha kwa makundi yasiyo ya kiserikali, lakini mipango yote hiyo imeshindwa kutekelezeka kivitendo.
Mpango unaopendekezwa na Washington ni pamoja na Hizbullah kupokonywa silaha kikamilifu, kutumwa jeshi la Lebanon katika eneo la kusini, ahadi ya utawala wa Israel ya kujiondoa katika nukta tano zinazokaliwa kwa mabavu, kutatuliwa masuala ya mpaka na madai ya kuimarisha mamlaka ya kujitawala taifa. Hata hivyo malengo hayo yanahudumia zaidi maslahi ya utawala wa Israel na Marekani kuliko kitu kingine chochote. Kupokonywa silaha bila kusitishwa uchokozi wa Israel, ahadi zenye masharti na kutokuwepo dhamana ya usalama inayoaminika, ni baadhi ya mambo yanayofanya mpango huu kutiliwa shaka. Changamoto zinazoukabili mpango huo ni pamoja na:

1. Mgawanyiko wa kimadhehebu: Kuidhinishwa mpangohuo katika baraza la mawaziri la Lebanon bila kuwepo mawaziri wa Kishia kunakiuka desturi za kisiasa za Lebanon na kuzidisha mivutano ya kimadhehebu. Hizbullah na Harakati ya Amal zinauchukulia mpango huo kuwa kinyume cha sheria, na jamii ya Mashia wa nchi hiyo wanalichukulia suala la upokonyaji silaha kama tishio la uwepo wao nchini. Uzoefu wa mgogoro wa 2008 pia unaonyesha kuwa hatua hizo zinaweza kusababisha migogoro ya ndani.
2. Udhaifu wa jeshi la Lebanon: Jeshi linakidhi sehemu ndogo tu ya mahitaji yake na halina uwezo wa kutosha wa kulinda nchi. Mgogoro wa kiuchumi umezidisha udhaifu huo. Kwa hivyo, jukumu la jeshi kuendesha zoezi la upokonyaji silaha haliwezi kutekelezeka kivitendo.
3. Kudhoofisha mamlaka ya kitaifa: Katika hali ambayo Israel inashambulia ardhi ya Lebanon kila siku na kuteka maeneo zaidi, kupokonywa silaha Hizbullah kunamaanisha kufutwa kwa nguvu pekee inayolinda nchi.
Mpango wa kuipokonya silaha Hizbulah ni sehemu ya mkakati mkuu wa Marekani na Israel wa kudhoofisha mhimili wa muqawama kufuatia Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa. Kupitia mpango huo, utawala wa Israel inahalalisha mashambulizi yake dhidi ya Hizbullah na hivyo kuongeza hatari ya kushadidi migogoro ya kieneo. Vile vile uingiliaji wa kigeni na ujasusi wa droni na satelaiti unaofanywa na maadui pia umedhoofisha uhuru na mamlaka ya Lebanon. Changamoto zinazoweza kutokea baadaye kutokana na jambo hili ni pamoja na:
1. Kuendelea mkwamo wa kisiasa wa hivi sasa na mpango huo kubakia kwenye karatasi tu.
2. Mzozo wa ndani ikiwa serikali ya Lebanon itasisitiza kutekeleza mpango huo kwa nguvu.
3. Majadiliano ya kitaifa ya kuandaa mkakati wa ulinzi wa pamoja; ingawa hili linaonekana kutowezekana bila kusitishwa uchokozi wa Israel na kutolewa dhamana ya usalama ya kuaminika.
Mpango wa kuipokonya silaha Hizbullah sio tu kwamba hautekelezeki kutokana na ukiukaji wa makubaliano ya kikabila na kidini, ukosefu wa dhamana ya usalama na uingiliaji wa kigeni, bali pia unaiweka Lebanon katika hali ya ukosefu wa amani na uingiliaji zaidi wa kigeni. Hivyo ni wazi kuwa kabla ya uvamizi wa Israel kukomeshwa na dhamana ya kuaminika ya usalama kutolewa, silaha za muqawama kama mdhamini wa usalama wa taifa, litabakia kuwa suala lisiloweza kujadiliwa.