Wanamgambo wa RSF waafiki pendekezo la kusitisha vita Sudan
-
Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vya Sudan (RSF)
Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vya Sudan (RSF) vimetangaza kwamba vinakubali usitishaji vita uliopendekezwa na Kamati ya Kimataifa ya Pande Nne.
Taarifa iliyotolewa na wanamgambo hao wa RFS wanaotuhumiwa kutenda jinai dhidi ya binadamu imeeleza kuwa, vinataka usitishaji vita utekelezwe ili mchakato wa kisiasa uanze. Aidha wanamgambo hao wamesema wamekubali kusitisha vita ili kuruhusu misaada ya kibinadamu nchini humo.
RSF pia imesema iko tayari kufanya mazungumzo kuhusu kukomesha uhasama kati yake na Jeshi katika kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miaka miwili.
Hata hivyo jeshi la Sudan halijakubaliana na mapendekezo hayo yaliyowasilishwa na Marekani na nchi za kiarabu.
Wiki hii msemaji wa Ikulu ya White House alisisitiza kwamba Marekani inaendelea "kushiriki kikamilifu" katika kutafuta suluhisho la mgogoro nchini Sudan, pamoja na washirika wake: Misri, Saudi Arabia, na Umoja wa Falme za Kiarabu.
"Tumewasilisha pendekezo la pingamizi kwa serikali ya Marekani. Kundi la wanamgambo wa RSF linapaswa kuvunjwa. Linapaswa kutangazwa kama kundi la kigaidi." "Na viongozi wake lazima wafikishwe mbele ya sheria. Hilo ndilo suluhisho pekee lililopo," anasisitiza Mohamed Osman Akasha, balozi wa Sudan jijini Nairobi.
Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yamesema yana wasiwasi mkubwa kufuatia taarifa za kuongezeka kwa ukatili na madhila dhidi ya raia wanaokimbia mji wa El Fasher, Sudan.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imesema imekuwa ikipokea taarifa nyingi zinazoongezeka kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za raia, huku mapigano yakiendelea katika jimbo la Darfur Kaskazini.
RSF, chini ya uongozi wa Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, iliteka El Fasher, makao makuu ya Darfur Kaskazini wiki iliyopita, katika mojawapo ya vipindi vya umwagaji damu zaidi vya vita vinavyoendelea kati ya kikundi hicho cha waasi na jeshi la Sudan, vilivyoanza Aprili 2023 na kusababisha maangamizi makubwa nchini Sudan.