Araghchi: Tunaendelea kufungua milango ya masoko ya kimataifa kwa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i132890-araghchi_tunaendelea_kufungua_milango_ya_masoko_ya_kimataifa_kwa_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, wizara yake inaendelea na jitihada zake za kidiplomasia za kufungua milango ya masoko ya kimataifa kwa ajili ya Iran na kuwasahilishia mambo wale wote wanaojishughulisha na masuala ya kiuchumi.
(last modified 2025-11-07T07:21:00+00:00 )
Nov 07, 2025 03:47 UTC
  • Araghchi: Tunaendelea kufungua milango ya masoko ya kimataifa kwa Iran
    Araghchi: Tunaendelea kufungua milango ya masoko ya kimataifa kwa Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, wizara yake inaendelea na jitihada zake za kidiplomasia za kufungua milango ya masoko ya kimataifa kwa ajili ya Iran na kuwasahilishia mambo wale wote wanaojishughulisha na masuala ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo mjini Hamedan, magharibi mwa Iran na huku akitoa maelezo kuhusu mafanikio ya kidiplomasia ya wizara yake katika masuala ya kiuchumi amesema: Tumefanya juhudi kubwa za kufungua milango ya masoko ya kimataifa kwa Iran na kuwarahisishia mambo wafanyabiashara na watu wote wanaojishughulisha na masuala ya kiuchumi.

Amesema: "Sikatai kuwa kuna vikwazo; vikwazo vipo kweli, lakini wafanyabiashara wa Iran wanasema kuwa watafanya kazi zao bila ya kuzuiwa na vikwazo hivyo, wanachotaka ni kusuluhishwa tu matatizo yetu ya ndani. Vikwazo vya kigeni vipo, sawa, lakini anachotaka mfanyabiashara wa Iran ni kuondolewa tu vikwazo vya ndani katika harakati zake."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema: Lazima tuelewe kwamba mfanyabiashara anayefanya kazi chini ya masharti magumu ya vikwazo kwa kweli anafanya kazi kimiujiza. Anasafirisha nje bidhaa, anauza, ananunua na kuhamisha pesa zake chini ya masharti haya ya vikwazo, kupitia njia ambazo wakati mwingine ni hatari. Kwa mtazamo wangu, watu kama hawa wanapaswa kutiwa moyo; baadhi yao hata wanastahili kupokea medali na kupongezwa kitaifa.

Sayyid Araghchi pia amesema, huwa tunafanya mikutano ya kutangaza zaidi bidhaa za Iran na kuwaalika pia mabalozi lengo likiwa ni kutoa fursa kwa maafisa na wanaharakati wa kiuchumi wa pande zote kukutana pamoja na kutambua uwezo na fursa zilizopo za ushirikiano wa kiuchumi.