Wanawake 400 wa Kipalestina na watoto wangali wanashikiliwa mateka na Israel
-
Wanawake 400 wa Kipalestina na watoto wangali wanashikiliwa mateka na Israel
Mashirika matatu ya Kipalestina yanayohusiana na masuala ya mateka yametangaza kuwa, utawala ghasibu wa Israel unawashikilia Wapalestina 9,250 wakiwemo wanawake 49 na watoto 350 katika jela zake.
Kamati ya Masuala ya Mateka na Watu Wanaoachiwa huru, Klabu ya Wafungwa wa Palestina na Taasisi ya Masuala ya Wafungwa na Haki za Kibinadamu ya "Al-Dhameer" zimetangaza katika taarifa ya pamoja kwamba, kulingana na takwimu za utawala wa kizayuni wa Israel ni kuwa, hadi Novemba 2025, idadi ya mateka katika jela za utawala huo ghasibu ilifikia 9,250.
Taasisi hizo za Palestina zimeongeza kuwa, takwimu hizi hazijumuishi mateka wanaoshikiliwa katika vituo vya kijeshi vya utawala huo ghasibu. Miongoni mwa wafungwa hao, 49 ni wanawake na 350 ni watoto.
Mateka hao wanashikiliwa katika mazingira yasiyo ya kibinadamu ambapo haki zote za kimsingi za binadamu zinakiukwa, na sheria za kimataifa na Mikataba ya Geneva inakiukwa kwa mpangilio maalumu dhidi ya wafungwa.
Wakati huo huo ripoti zinasema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya ugaidi ulioratibiwa dhidi ya mateka wa Kipalestina iliowaachia huru na umezikataza familia za mateka hao kuwaandalia mapokezi ya aina yoyote ndugu zao.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) pia imesisitiza katika taarifa yake kuwa, unyanyasaji wa kutisha na unaoendelea katika magereza ya Israel dhidi ya mateka hao mashujaa ni jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu na kuna ulazima Umoja wa Mataifa na taasisi za haki za binadamu kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kukomesha vitendo hivyo visivyo vya kibinadamu vya Wazayuni na kuwawajibisha wahusika.