Rais mzee zaidi duniani aapishwa kuongoza Cameroon kwa muhula wa nane
Kiongozi wa muda mrefu wa Cameroon, Paul Biya, ameapishwa kwa muhula mpya wa miaka saba kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita, ambao mpinzani wake ameutaja kama "mapinduzi ya kikatiba".
Akihutubia Bunge siku ya Alkhamisi, rais huyo mzee zaidi duniani aliahidi kubakia mwaminifu kwa imani ya watu wa Cameroon na kuahidi kufanya kazi kwa ajili ya nchi "iliyoungana, tulivu na yenye ustawi".
Baraza la katiba la Cameroon lilimtangaza Rais aliyeko madarakani Paul Biya mwenye umri wa miaka 92 kuwa mshindi wa kiti cha urais kwa karibu asilimia 54% ya kura.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Cameroon, ushiriki wa wapiga kura ulikuwa asilimia 57.76, huku asilimia 42.24 wakijiondoa katika mchakato wa kupiga kura.
Hata hivyo, matokeo haya yanapingana na madai ya mgombea wa upinzani Issa Tchiroma, ambaye kabla ya matokeo rasmi kutangazwa, alijitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo.
Maeneo mbalimbali ya Cameroon yalishuhudia maandamano ya watu wenye hasira wanaopinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Paul Biya.
Akiwa yuko madarakani kwa takribani miaka 43, Paul Biya (92) sasa ataongoza kwa muhula wa nane wa miaka mingine saba. Mrengo wa upinzani nchini Cameroon umekuwa ukikosoa uongozi wake na kumtuhumu kushindwa kuiongoza nchi.
Paul Biya mara kwa mara husafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, na mwaka jana uvumi ulienea kwamba alikuwa amefariki dunia, uvumi ambao serikali iliukanusha vikali hadharani.