Rais Pezeshkian: Migawanyiko na mifarakano baina ya Waislamu inaunufaisha Uzayuni wa dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i132910-rais_pezeshkian_migawanyiko_na_mifarakano_baina_ya_waislamu_inaunufaisha_uzayuni_wa_dunia
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, migawanyiko na mifarakano baina ya Waislamu ndilo jambo hasa wanalolitamani maadui wa Uislamu.
(last modified 2025-11-07T11:52:14+00:00 )
Nov 07, 2025 11:52 UTC
  • Rais Pezeshkian: Migawanyiko na mifarakano baina ya Waislamu inaunufaisha Uzayuni wa dunia

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, migawanyiko na mifarakano baina ya Waislamu ndilo jambo hasa wanalolitamani maadui wa Uislamu.

Rais Pezeshkian ameyasema hayo mjini Sanandaj mbele ya hadhara ya maulamaa na viongozi wa dini wa madhehebu ya Sunni wa mkoa wa Kordestan magharibi mwa Iran na kusisitiza kwamba umoja, imani, na kurejea kwenye udugu wa Kiislamu ndivyo vitu pekee vitakavyouwezesha Ulimwengu wa Kiislamu kukabiliana na njama za Marekani, Israel, na Uzayuni wa dunia.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametahadharisha kuwa, migawanyiko ya ndani inanufaisha na kukidhi maslahi ya madola yenye uadui.

"Migawanyiko hii ndiyo ambayo Israel, Marekani, na Uzayuni wa dunia zinaifuatilia ili kuufanya Umma wa Kiislamu ushughulishwe na mizozo ya ndani wakati wao wanafanya uvamizi na uchokozi wowote wanaotaka" ameeleza Pezeshkian.

Rais wa Iran ameielezea Israel kuwa ni "kijitawala kidogo kilichoanzishwa kupitia uchokozi" ambacho kimeweza kubaki na kusababisha matatizo kwa Ulimwengu wa Kiislamu kutokana na migawanyiko iliyopo baina ya Waislamu.

"Ikiwa umoja na mshikamano utatawala baina yetu, hakuna dola litakalothubutu kuzifanyia tamaa ardhi za Kiislamu," ameeleza Pezeshkian na kuongeza kuwa mifarakano ya ndani ndio chimbuko la masaibu mengi yanayoupata Ulimwengu wa Kiislamu, na kurejea kwenye imani, udugu, na kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu ndiko pekee kutakowezesha kuushinda mzunguko huo.

Rais wa Iran ameeleza masikitiko yake kwa kusema, msingi wa udugu, ambao ni usuli wa dini na maadili umesahaulika, na hivyo kuwawezesha maadui kuutumia udhaifu huo.

"Kusahau ukweli huu kumeuweka mbali Umma wa Kiislamu na mshikamano, na kufungua mlango wa ushawishi wa kigeni. Kurejea kwenye msingi huu wa Qur'ani kunamaanisha kujenga upya umoja", amesisitiza Rais Pezeshkian.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasili Sanandaj, makao makuu ya Mkoa wa Kordistan siku ya Alkhamisi na kukutana na makundi na matabaka mbali mbali ya wananchi pamoja na wanaharakati kutoka sekta tofauti.../