Ni yapi matokeo ya mkutano wenye utata wa Trump na Putin?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129610-ni_yapi_matokeo_ya_mkutano_wenye_utata_wa_trump_na_putin
Hatimaye, baada ya kusubiri kwa muda mrefu na uvumi kuhusu mkutano kati ya Marais Donald Trump wa Marekani na Vladimir Putin wa Russia kuhusu vita vya Ukraine, mkutano huo hatimaye ulifanyika Ijumaa, Agosti 15 huko Alaska.
(last modified 2025-08-16T11:27:09+00:00 )
Aug 16, 2025 11:27 UTC
  • Ni yapi matokeo ya mkutano wenye utata wa Trump na Putin?

Hatimaye, baada ya kusubiri kwa muda mrefu na uvumi kuhusu mkutano kati ya Marais Donald Trump wa Marekani na Vladimir Putin wa Russia kuhusu vita vya Ukraine, mkutano huo hatimaye ulifanyika Ijumaa, Agosti 15 huko Alaska.

Mkutano huo bila shaka uliambatana na mbwembwe na vioja vingi vya nguvu vya kumkaribisha Trump, kama vile kuruka ndege za kivita aina ya B-2 kwenye eneo la mkutano katika Uwanja wa Ndege wa Elmendorf-Richardson katika mji wa Anchorage. Baada ya mkutano huo uliodumu kwa takriban saa tatu, marais wa Marekani na Russia walishiriki katika mkutano na waandishi wa habari.

Baada ya mazungumzo na Vladimir Putin, Donald Trump alisema mkutano huo ulikuwa na tija ambapo wahusika walikubaliana juu ya mambo mengi, na kwamba ni machache tu ambayo hayakujadiliwa.

Rais Vladimir Putin pia alitathmini mazungumzo ya saa tatu na mwenzake wa Marekani huko Alaska kuwa yenye tija na manufaa na kusema: "Utatuzi wa mzozo wa Ukraine ni moja ya masuala makuu yaliyojadiliwa katika mkutano na Trump." 

Rais wa Russia pia alisema: "Tunatazamia kuwa Kiev na miji mikuu ya Ulaya itaelewa haya yote kwa njia ya kujenga na haitaweka vikwazo vyovyote wala kufanya juhudi za kuvuruga maendeleo yaliyopatikana, kwa uchochezi au njama za nyuma ya pazia."

Inaonekana kwamba Trump, ambaye tangu mwanzo wa urais wake amekuwa akidai kwamba anaweza kumaliza vita vya Ukraine katika siku moja, ameshindwa vibaya katika uwanja huo ambapo sasa mkutano wake na Putin katika jimbo la Alaska umekuwa hatua ya mabadiliko na njia ya kuokoa ahadi yake hiyo. Kwa sababu hii, Trump alikuwa ametangaza wazi kabla ya mkutano huo kwamba angeondoka mkutanoni ikiwa haungekwenda kama alivyotarajia. Hata hivyo, baada ya mkutano wa saa tatu na Putin, ameonekana kuridhika.

Kwa upande mwingine, mkutano huu umekuwa na mafanikio mengi kwa Putin. Kwanza kabisa ni kwamba, baada ya muda mrefu, amesafiri kwenda Marekani licha ya hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, na hili linachukuliwa kuwa kutambuliwa rasmi nafasi yake ya madaraka na viongozi wa Washington. Kwa upande mwingine, Marekani imechelewesha baadhi ya vikwazo dhidi ya Russia na inapanga kufuta vingine, ambapo ni mafanikio mengine kwa Moscow. Muhimu zaidi ni kwamba ushahidi unaonyesha kuwa Trump anakusudia kumaliza vita vya Ukraine kwa kuipa Russia sehemu ya Ukraine, hasa eneo la Donbass, ambalo linajumuisha Luhansk na Donetsk, ambalo kwa hakika litakuwa pigo kubwa kwa Kiev baada ya miaka minne ya vita.

Mazungumzo ya pande mbili kati ya Trump na Putin huko Alaska

Wakati huo huo, vyombo vya habari na baadhi ya wanasiasa wa nchi za Magharibi wamefuatilia kwa makini mkutano wa Marais wa Marekani na Russia wakisema Trump amemkaribisha Putin kwa zulia jekundu kwa ajili ya kubembeleza aafikiane naye katika baadhi ya mambo. Kuhusiana na hilo John Bolton, mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani amesema Vladmir Putin ndiye mshindi wa wazi wa mkutano huu.

Suala muhimu ni mtazamo wa Ukraine na nchi za Ulaya juu ya mkutano huu, na kama ilivyotarajiwa, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amekosoa vikali mkutano huo na matokeo yake. Amesema, Vladimir Putin alishiriki katika mkutano huo akiwa na malengo matatu makuu na akafanikiwa kuyafikia yote. Amesema: "Putin alihitajia picha moja tu ya mkutano wake na Trump, picha hii ilimtosha kufaidika kisiasa."  Zelensky pia amedai kwamba Putin alikuwa anatafuta njia ya kujitoa katika hali ya kutengwa na kupata uhalali wa kimataifa, ambapo mkutano wake na rais wa Marekani umempa fursa hiyo. Akizungumzia vitisho vya Trump vya kuweka vikwazo vikali dhidi ya Russia na wanunuzi wa mafuta ya nchi hii, Rais wa Ukraine amesema: "Kwa mkutano huu, Putin ameweza kuahirisha vikwazo; vikwazo ambavyo ni vizito sana na tunasubiri kwa hamu utekelezaji wake."

Taathira zinazoweza kuonekabna baadaye kutokana na mkutano wa Trump na Putin juu ya vita vya Ukraine zinaweza kuorodheshwa kama ifuatavyo: 

1. Kuongezeka mashinikizo ya kusitisha mapigano kutoka kwa Marekani. Kuhusu suala hili, Trump ametoa wito wa kusitishwa vita mara moja na akapendekeza mkutano wa pande tatu na Zelensky. Msimamo huu unaweza kuongeza mashinikizo ya kimataifa kwa Russia na Ukraine ili ziketi kwenye meza ya mazungumzo ya kumaliza vita.

2. Mabadiliko katika msimamo wa Marekani: Kuna uwezekano kwamba sera ya Marekani kuhusu Ukraine itabadilika kutoka usaidizi mkubwa wa kijeshi hadi kuzingatia mazungumzo na makubaliano, mabadiliko ambayo yanaweza kuathiri uwiano wa nguvu katika uwanja wa vita.

3. Kujaribu kufikia makubaliano kuhusu ardhi: Inasemekana kwamba wakati wa mkutano, majadiliano yalitolewa kuhusu maeneo yanayodhibitiwa na Russia nchini Ukraine, lakini hakuna makubaliano yaliyofikiwa. Mazungumzo hayo yanaweza kuwa msingi wa makubaliano ambayo yatakabidhi sehemu ya ardhi ya Ukraine kwa Russia, ambayo, bila shaka, yataambatana na hisia kali kutoka Umoja wa Ulaya na Ukraine.

4. Kuongezeka mvutano kati ya nchi za Ulaya: Nchi za Ulaya kama Ujerumani na Ufaransa zinapinga makubaliano yoyote ambayo yatabadilisha mipaka ya nchi. Iwapo Marekani itafikia makubaliano na Russia katika uwanja huo, huenda yakaibua nyufa katika muungano wa Magharibi dhidi ya Russia.

Kwa ujumla, mkutano wa Trump na Putin huko Alaska zaidi ulikuwa aina fulani ya "kuanzisha upya" mahusiano ya Marekani na Russia kuliko kufikia makubaliano yenye natija ya mwisho. Kwa kuzingatia anga ya kimataifa, mkutano huu unaweza kuwa utangulizi wa mazungumzo mazito zaidi katika siku zijazo. Mkutano huu bado haujakuwa na taathira za moja kwa moja na za haraka katika vita vya Ukraine, lakini kama ishara muhimu ya kisiasa, unaweza kubadilisha mkondo wa siku zijazo. Ikiwa mazungumzo yataendelea na Trump kuchukua nafasi ya mpatanishi, kuna uwezekano wa kumalizika vita kupitia suluhu ya kidiplomasia, na bila shaka, kwa kugharamika pande husika.