DRC yapinga kupelekwa balozi mdogo wa Kenya mjini Goma
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129636-drc_yapinga_kupelekwa_balozi_mdogo_wa_kenya_mjini_goma
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imepinga hatua ya Kenya ya kumteua balozi mdogo anayetazamiwa kutumwa katika mji wa Goma ulioko mashariki mwa DRC, ikiuelezea uamuzi huo kuwa "usiofaa".
(last modified 2025-08-17T11:37:05+00:00 )
Aug 17, 2025 11:37 UTC
  • DRC yapinga kupelekwa balozi mdogo wa Kenya mjini Goma

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imepinga hatua ya Kenya ya kumteua balozi mdogo anayetazamiwa kutumwa katika mji wa Goma ulioko mashariki mwa DRC, ikiuelezea uamuzi huo kuwa "usiofaa".

Serikali ya Kinshasa inayoongozwa na Rais Felix Tshisekedi imesema kumteua balozi mdogo katika jiji hilo ni sawa na kutoheshimu mamlaka ya kujitawala nchi hiyo, na kunaweza kuonekana kama kuhalalisha uvamizi wa kundi la waasi wa M23.

Aidha, imesema Kenya haikuwasiliana na Kinshasa kabla ya kutoa tangazo hilo, kama inavyotakiwa na sheria za kimataifa na miongozi ya kidiplomasia.

Goma, mji ulioko mashariki mwa Kongo, umekuwa kitovu cha mzozo kati ya serikali ya Kongo na kundi la waasi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Nchi jirani za DRC, ikiwa ni pamoja na Rwanda, Burundi, Uganda, na Kenya, zote zimekuwa na askari mashariki mwa DRC kama sehemu ya juhudi za kikanda za kukomesha mapigano katika eneo hilo.

Christian Moleka, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Kongo DR, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba, uteuzi huo wa balozi mdogo wa Kenya mjini Goma unaweza kuwa na athari za kikanda. Amesema huenda ukalemaza zaidi imani ya Kinshasa kwa Nairobi, katika hali ambayo Kenya imekuwa ikionekana ikijikurubisha zaidi kwa Rwanda chini ya Rais William Ruto, na kudhoofisha juhudi za kikanda za kuleta amani.

Eneo la Mashariki mwa DRC limekumbwa na ghasia za makundi mengi yenye silaha kwa takriban miaka 30 sasa. Jumuiya ya Afrika Mashariki imechukua hatua kadhaa za kujaribu kurejesha amani katika eneo hilo, baada ya Kongo DR kuwa mwanachama rasmi wa jumuiya hiyo mwaka 2022.