Magaidi kadhaa waangamizwa katika operesheni ya IRGC kusini mashariki mwa Iran
Vikosi vya usalama vya Iran vimesambaratisha mtandao mkubwa wa magaidi wakufurishaji na kuua kadhaa miongoni mwao, mbali na kunasa silaha na mabomu kadhaa katika mkoa wa kusini mashariki wa Sistan na Baluchestan.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza habari hiyo na kueleza kuwa, limevunja vikundi viwili vya magaidi katika mkoa wa Sistan na Baluchestan katika operesheni kabambe ya leo Jumapili.
"Vikosi vya Makao Makuu ya Quds, kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama na kijasusi, vimefanikiwa kubaini na kuharibu maficho ya magaidi kaskazini na kusini mwa mkoa wa Sistan na Baluchestan," IRGC imesema katika taarifa yake.
Katika operesheni hizi tofauti, magaidi sita waliokuwa wakipanga kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga na hujuma waliuawa. Taaria hiyo imeongeza kuwa, magaidi wengine kadhaa wametiwa mbaroni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, takriban kilo 25 za mada za miripuko na mabomu ziligunduliwa na kutwaliwa katika operesheni hizo.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) hivi karibuni lilivunja mtandao mwingine wa kigaidi unaohusishwa na Marekani na Israel katika Mkoa wa Mazandaran kaskazini mwa Iran, na kufichua njama zaidi za maadui za kuvuruga utulivu wa Iran.
Wakuu wa Iran wamekuwa wakiilaumu Marekani na washirika wake kwa kusaidia makundi ya kigaidi yanayolenga kuvuruga usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.