Iran yazindua kliniki 9 kote nchini za kutibu majeraha kwa kutumia plasma
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129400
Mohammad Eslami, Makamu wa Rais na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) ametangaza kuzinduliwa kliniki tisa maalumu kote nchini zinazotumia plasma kutibu majeraha.
(last modified 2025-08-11T09:05:59+00:00 )
Aug 11, 2025 09:05 UTC
  • Iran yazindua kliniki 9 kote nchini za kutibu majeraha kwa kutumia plasma

Mohammad Eslami, Makamu wa Rais na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) ametangaza kuzinduliwa kliniki tisa maalumu kote nchini zinazotumia plasma kutibu majeraha.

Eslami alisema jana katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika kliniki mpya katika Hospitali ya Rasul Akram mjini Tehran kwamba: Vituo vipya vitano vimezinduliwa leo. "Hivi sasa, kuna vituo vinane vya matibabu ya majeraha vinavyofanya kazi Tehran na kimoja huko Sabzevar, mji wa kaskazini-mashariki mwa Iran, vinavyotoa huduma kwa wagonjwa", aliongeza kusema Eslami. 

Amesisitiza kuwa  afya na usalama wa chakula ni vipaumbele vya juu vya Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran na kuongeza: "Tumepanga kupanua zaidi matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na dawa na kuifanya teknolojia hiyo ipatikane katika sekta tofauti.

Mohammad Eslami amesema kuwa teknolojia ya plasma ya baridi imeonyesha matokeo ya kutia matumaini na chanya katika kutibu majeraha.