Watu 25 wafukiwa na kifusi Tanzania wakati shughuli za ukarabati mgodi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129518
Watu 25 wamefukiwa na kifusi katika mgodi mdogo wa dhahabu unaomilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi, uliopo Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Shinyanga, mkoani Shinyanga nchini Tanzania, baada ya mgodi huo kutitia wakati wa zoezi la ukarabati wa maduara.
(last modified 2025-08-14T09:09:13+00:00 )
Aug 14, 2025 06:53 UTC
  • Mgodi wa Shinyanga
    Mgodi wa Shinyanga

Watu 25 wamefukiwa na kifusi katika mgodi mdogo wa dhahabu unaomilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi, uliopo Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Shinyanga, mkoani Shinyanga nchini Tanzania, baada ya mgodi huo kutitia wakati wa zoezi la ukarabati wa maduara.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Mkoa wa Shinyanga imefika eneo la tukio kutoa pole na kushiriki katika zoezi la uokoaji, likiwa chini ya usimamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wachimbaji wa mgodi huo.

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kutitia kwa ardhi wakati shughuli za ukarabati zikiendelea. Hadi sasa, watu saba kati ya 25 wameokolewa wakiwa hai, huku jitihada za kuwaokoa waliobaki zikiendelea kwa nguvu zote.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro akiwa kwenye eneo la uokozi amesema baada ya kufika eneo la tukio aliomba wananchi wawe watulivu wakati kazi ya uokozi ikiendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita akizungumza na wananchi na wafanyakazi wa eneo hilo, alitoa salamu za pole na kushukuru kazi waliyoanza kuifanya ya uokozi.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Joseph Shahibu alidai kuna vijana wanaoweza kusaidia kazi ya uokozi hivyo aliomba waruhusiwe washiriki.