Al-Sisi: Misri haitafumbia macho haki yake ya maji
Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri, amesema kwamba mtu yeyote anayedhani kwamba Misri itafumbia macho haki yake ya kunufaika na maji ya Mto Nile anakosea.
Amesema suala la maji linatumika kama sehemu ya kampeni ya kufikia malengo mengine kwa madhara ya Misri. Rais Al-Sisi ameyasema hayo katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Rais Yoweri Museveni wa Uganda katika Ikulu ya Al-Ittihadiya na kuongeza kuwa suala la maji ya Mto Nile ni mada ya mazungumzo ya muda mrefu na Rais wa Uganda.
Al-Sisi amesisitiza umuhimu wa maji na maendeleo kwa nchi za Bonde la Mto Nile na kuongeza: "Misri haipingi maendeleo yoyote kwa washirika na ndugu zetu katika nchi za Bonde la Mto Nile, bali wasiwasi pekee wa Misri ni kwamba maendeleo hayo yanaathiri kiwango cha maji kinachofika Misri."
Rais wa Misri amesema: "Tunataka kufanya kazi pamoja ili kufikia utulivu katika nchi yetu. Misri haina vyanzo vingine vya maji na haipati mvua kubwa. Tukifumbia macho sehemu hii, ina maana kwamba tumepoteza maisha."
Al-Sisi amefafanua kuwa Misri haipingi matumizi ya maji ya Mto Nile kwa ndugu zake, iwe ni katika maendeleo, kilimo au uzalishaji wa umeme. Amesisitiza kuwa Misri inaheshimu juhudi za kamati ya watu saba inayoongozwa na Uganda kufikia muafaka kati ya nchi zote za Bonde la Mto Nile.
Amesema: Wamisri wana wasiwasi kuhusu suala hili, lakini wajibu wake kama rais ni kushauriana na marais wengine ili kutafuta suluhisho ambalo halitaathiri maisha ya Wamisri.
Rais wa Misri ameongeza: "Ninawahakikishia Wamisri kwamba kamwe hatutaruhusu maji ya raia milioni 105, pamoja na wageni milioni 10 nchini kuharibiwa."
Naye Rais Museveni wa Uganda amesema kuwa nchi yake na kamati ya watu saba zinafanya juhudi za kuhakikisha kuwa mzozo uliopo kuhusiana na maji ya Mto Nile unatatuliwa kwa njia ya amani kwa manufaa ya mataifa yote ya eneo.