Je, siasa za serikali ya Modi zimewatenga Waislamu wa India?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129520
Waislamu wa India, ambao ni zaidi ya watu milioni 200, katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakikabiliwa na changamoto zinazoongezeka katika uwanja wa haki za uraia, usalama wa kijamii na ushiriki wa kisiasa.
(last modified 2025-08-14T07:41:22+00:00 )
Aug 14, 2025 07:41 UTC
  • Je, siasa za serikali ya Modi zimewatenga Waislamu wa India?

Waislamu wa India, ambao ni zaidi ya watu milioni 200, katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakikabiliwa na changamoto zinazoongezeka katika uwanja wa haki za uraia, usalama wa kijamii na ushiriki wa kisiasa.

Tangu iingie madarakani mwaka 2014, serikali ya Narendra Modi Waziri Mkuu wa India na kiongozi wa chama cha Hindu Bharatiya Janata Party (BJP) imetekeleza sera ambazo zinaelezwa na waangalizi wengi wa ndani na kimataifa kuwa ni mfululizo wa hatua za ubaguzi, upendeleo na chuki dhidi ya Uislamu. Sera hizi sio tu zimeathiri maisha ya kila siku ya Waislamu, bali pia zimebadilisha muundo wa kijamii na kisiasa wa India.

Itikadi ya "Hindutva" ambayo inaunda msingi wa kiitikadi wa BJP inasisitiza ubora wa kitamaduni na kisiasa wa Wahindu, inaunganisha utambulisho wa kitaifa wa India na tamaduni na dini ya Kihindu, na inawatazama walio wachache wa kidini, hasa Waislamu, kama "wengine" na "wageni". Tangu Modi aingie madarakani mwaka 2014, mtazamo huu umekuwa ukiimarika zaidi katika sera za serikali. Mtazamo huu umeunda msingi wa sera zinazolenga kupunguza ushawishi wa Waislamu katika miundo ya kijamii na kisiasa ya India. Kuondolewa hadhi maalum ya Kashmir kwa kufutwa Kifungu cha 370 cha Katiba ya India ni mfano wa wazi wa jaribio la serikali la kubadilisha muundo wa idadi ya watu katika maeneo yenye Waislamu wengi.

Sheria nyingine muhimu ambayo imeibua wasiwasi mkubwa ndani na nje ya India ni Sheria ya Marekebisho ya Uraia (CAA) na Daftari la Kitaifa la Raia (NRC). CAA inaruhusu wahamiaji wasio Waislamu kutoka nchi jirani kupata uraia wa India, wakati Waislamu wananyimwa fursa hiyo. Sheria hii, sambamba na mpango wa NRC unaohitaji uthibitisho wa uraia, imeweka Waislamu katika hatari ya kutokuwa na utaifa na hatimaye kufukuzwa nchini. Mpango huu unawataka raia kutoa uthibitisho wa uraia wao. Waislamu wengi hasa wa maeneo maskini hawana hati hizo na kwa hivyo wanakabiliwa na hatari ya kupokonywa utaifa.

Kuharibiwa Msikiti wa Babri na Wahindu wenye itikali za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu

Katika miaka ya hivi karibuni, uharibifu wa misikiti, nyumba na biashara zinazomilikiwa na Waislamu umeongezeka wakati wa machafuko ya mijini na hatua za serikali dhidi yao. Uharibifu wa Msikiti wa Babri uliofanywa na vikundi vya itikadi kali za Kihindu na kutochukuliwa hatua madhubuti na serikali katika uwanja huo ni ishara ya wazi kuwa serikali haijali haki za kidini za Waislamu. Katika baadhi ya majimbo, nyumba na biashara za Waislamu zimeharibiwa kwa visingizio mbalimbali. Pia, uharibifu wa misikiti na maeneo ya ibada ya Waislamu wakati wa migogoro ya kikabila na kidini, bila majibu madhubuti kutoka kwa serikali, umeibua wasiwasi mkubwa nchini India. Miji mbalimbali nchini humo imeshuhudia wimbi kubwa la maandamano dhidi ya uharibifu wa nyumba na maduka ya Waislamu yaliyoamriwa kuvunjwa na mamlaka za mitaa katika jimbo la Uttar Pradesh kaskazini mwa India mnamo Juni 2022. Katika kupinga kile walichokiita "siasa za dhulma", waandamanaji walitaka kusitishwa mara moja uharibifu wa makazi na biashara za Waislamu katika nchi hiyo. Wakosoaji wanasema kuwa lengo la uharibifu wa mali ya Waislamu, unaojulikana kama "Uadilifu wa Buldoza", ni kuwakandamiza na kuwatia hofu Waislamu, jambo ambalo limeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni.

Viongozi wa BJP na Narendra Modi mwenyewe mara kwa mara wametumia matamshi katika hotuba za uchaguzi ambayo yameelezwa na vyama vya upinzani kuwa ya chuki dhidi ya Uislamu na yanayoibua migawanyiko, ambapo yanawadhihirisha Waislamu kama tishio kwa jamii ya Wahindi. Kusambazwa video kwenye mitandao ya kijamii zinazohusisha Waislamu na ufisadi au vurugu ni sehemu ya siasa hizo za chuki na mfano wa propaganda za serikali ya India, ambazo zimechochea mivutano ya kidini nchini.

Vyama vya upinzani, wanaharakati wa haki za binadamu na mashirika ya kimataifa yameonya mara kwa mara dhidi ya sera za serikali ya Modi. Chama cha Indian National Congress Party, ambacho ni chama kikubwa zaidi cha upinzani, kimeituhumu serikali kwa kuchochea migawanyiko, kueneza chuki na kukiuka wazi kanuni za serikali kutokuwa na udini. Pia, mashirika ya kutetea haki za binadamu, likiwemo la Human Rights Watch, yameeleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la ghasia za kidini na ubaguzi wa kimfumo dhidi ya Waislamu nchini India na yameonya mara nyingi kuhusu ongezeko la ukatili wa kidini na ubaguzi wa kimfumo dhidi ya Waislamu. Viongozi wa kidini katika nchi za Kiislamu pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya Waislamu wa India.

Siasa za serikali ya Modi, zenye msingi wa Hindutva na utaifa wa kupindukia mipaka,kuanzia sheria za kibaguzi hadi mijadala ya chuki dhidi ya Uislamu, zimefanya hali ya kijamii ya India kuwa ngumu zaidi kwa Waislamu na kuibua hali ya wasiwasi kwa wafuasi wa dini za wachache nchini humo. Waislamu wanaunda takriban asilimia 14 ya watu wa India ambao ni bilioni 1.4 na ndio dini kubwa zaidi ya wachache nchini humo. Ijapokuwa serikali ya Modi inapinga ukosoaji wa upinzani na tuhuma zinazotolewa na makundi ya haki za binadamu, lakini vitendo hivi sio tu vinakanyaga kanuni zinazopinga ubaguzi wa kidini na kuimarisha wingi wa jamii za India, bali pia vinahatarisha kuzidisha mivutano ya kidini na kudhoofisha mshikamano wa kitaifa. Aidha, sera hizi zinatilia shaka uaminifu wa India kama demokrasia kubwa zaidi duniani. Hivyo mustakabali wa India unategemea kurejea kwake kwenye kanuni za wingi wa kijamii, haki za kiraia na kuheshimu haki za walio wachache.