BNP kutangaza serikali mpya ya Bangladesh Jumapili, kuitaka India imrudishe Hasina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136618-bnp_kutangaza_serikali_mpya_ya_bangladesh_jumapili_kuitaka_india_imrudishe_hasina
Chama cha Taifa cha Bangladesh (BNP) kimetangaza kuwa kitaunda serikali mpya ifikapo kesho Jumapili, baada ya kupata ushindi wa kishindo wa theluthi mbili ya viti vya Bunge katika uchaguzi wa kwanza kufanyika nchini humo tangu mapinduzi ya Julai 2024 yaliyoing'oa madarakani serikali ya aliyekuwa waziri mkuu Sheikh Hasina.
(last modified 2026-02-16T16:36:20+00:00 )
Feb 14, 2026 09:55 UTC
  • BNP kutangaza serikali mpya ya Bangladesh Jumapili, kuitaka India imrudishe Hasina

Chama cha Taifa cha Bangladesh (BNP) kimetangaza kuwa kitaunda serikali mpya ifikapo kesho Jumapili, baada ya kupata ushindi wa kishindo wa theluthi mbili ya viti vya Bunge katika uchaguzi wa kwanza kufanyika nchini humo tangu mapinduzi ya Julai 2024 yaliyoing'oa madarakani serikali ya aliyekuwa waziri mkuu Sheikh Hasina.

"Serikali itakuwa imeundwa ifikapo Februari 15. BNP itaenda bungeni na vyama vyote," ameeleza Katibu Mkuu wa chama hicho Mirza Fakhrul Islam Alamgir katika mkutano na waandishi wa habari jana Ijumaa alipokuwa akitembelea jimbo lake kwenye wilaya ya kaskazini-magharibi ya Thakurgaon.

"Itakuwa serikali ya BNP. Na BNP itatekeleza ahadi na ilani yake ya uchaguzi; na masuala ambayo BNP ilitia saini katika Mkataba wa Julai kuhusu mageuzi yatatekelezwa hatua kwa hatua," amebainisha Alamgir. 

Mwenyekiti wa BNP Tarique Rahman ndiye anayetarajiwa kuwa mgombea wa chama hicho wa nafasi ya uwaziri mkuu. Rahman alishika wadhifa wa kiongozi wa chama baada ya kifo cha mama yake na waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Bangladesh, Khaleda Zia, kilichotokea mwezi Desemba.

Sambamba na uchaguzi mkuu, Wabangladesh walishiriki pia katika kura ya maoni ya "Mkataba wa Julai," uliopitishwa Oktoba iliyopita, kwa ajili ya mageuzi ya katiba, ambao umeungwa mkono kwa wingi mkubwa wa kura.

Mkataba huo una mapendekezo zaidi ya 80 yanayolenga kurekebisha utawala, ikiwa ni pamoja na mipaka ya mihula kwa waziri mkuu, kupanua mamlaka ya rais, kulinda uhuru wa mahakama, kuongeza uwakilishi wa wanawake, na haki pana za msingi.

Kwa mujibu wa Katiba ya Bangladesh, chama kinahitaji kupata viti 151 katika Bunge lenye viti 300 ili kuunda serikali. Katika uchaguzi uliofanyika siku ya Alkhamisi, BNP na washirika wake vilipata viti 212. Mshindani wake mkuu, kambi inayoongozwa na Jamaat-e-Islami, ilishinda viti 77.

Wakati huohuo, mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya BNP Salahuddin Ahmed amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Dhaka kwamba serikali mpya itaiomba rasmi India imrudishe aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo aliyetoroka Sheikh Hasina, ambaye anakabiliwa na adhabu ya kifo kwa kuamuru kufanywa ukandamizaji na vyombo vya usalama dhidi ya waandamanaji, uliopelekea kuuawa watu wasiopungua 1,400.

"Tutadai kurejeshwa kwake (Hasina) kulingana na sheria. Hili ni suala la Wizara ya Mambo ya Nje ya Bangladesh na Wizara ya Mambo ya Nje ya India. Tutadai kutoka kwa serikali ya India kwamba arudishwe ili afunguliwe mashtaka," amesisitiza Ahmed.../