Katika hotuba ya kuaga, Yunus asema kupinduliwa Hasina ulikuwa ukombozi kwa Bangladesh
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136744-katika_hotuba_ya_kuaga_yunus_asema_kupinduliwa_hasina_ulikuwa_ukombozi_kwa_bangladesh
Kiongozi wa mpito wa Bangladesh Muhammad Yunus, ametangaza kujiuzulu katika hotuba ya kuaga kwa taifa aliyotoa kabla ya kukabidhi mamlaka kwa serikali iliyochaguliwa.
(last modified 2026-02-18T03:04:35+00:00 )
Feb 18, 2026 03:04 UTC
  • Kiongozi wa mpito wa Bangladesh Muhammad Yunus
    Kiongozi wa mpito wa Bangladesh Muhammad Yunus

Kiongozi wa mpito wa Bangladesh Muhammad Yunus, ametangaza kujiuzulu katika hotuba ya kuaga kwa taifa aliyotoa kabla ya kukabidhi mamlaka kwa serikali iliyochaguliwa.

"Leo, serikali ya mpito inajiuzulu," ametamka mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwenye umri wa miaka 85 na akaongezea kwa kusema: "lakini bila kuacha lisitishwe zoezi la demokrasia, uhuru wa kusema, na haki za msingi ambalo limeanza."

Yunus alirudi Bangladesh mnamo Agosti 2024 kutoka kwenye uhamisho aliojiwekea mwenyewe, siku chache baada ya utawala wa Sheikh Hasina kupinduliwa na vuguvugu lililoongozwa na wanafunzi, na yeye mwenyewe kuitoroka nchi na kukimbilia India kwa helikopta.

"Ile ilikuwa siku ya ukombozi mkubwa," ameeleza Yunus na kuongezea kwa kusema: "ilikuwa siku ya furaha iliyoje! Wabangladeshi kote ulimwenguni walitokwa na machozi ya furaha. Vijana wa nchi yetu waliikomboa nchi kutoka kwenye mbano wa shetani."

Mwanauchumi huyo ameiongoza Bangladesh kama "mshauri mkuu" tangu wakati huo, na sasa amekabidhi madaraka baada ya kukipongeza Chama cha Taifa cha Bangladesh (BNP) na kiongozi wake, Tarique Rahman, kwa "ushindi mkubwa" waliopata katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.

"Watu, wapiga kura, vyama vya siasa, na taasisi za wadau waliohusishwa na uchaguzi huo wameweka mfano mzuri," ameeleza Yunus na akaongezea kwa kusema: "uchaguzi huu umeweka kipimo cha chaguzi zijazo."

Rahman, mwenye umri wa miaka 60, ambaye ni mkuu wa BNP anayetoka kwenye moja ya koo zenye nguvu kubwa zaidi za kisiasa nchini Bangladesh, ndiye atakayeliongoza taifa hilo la Asia Kusini lenye watu wapatao milioni 170.

Mbali na uchaguzi wa Bunge, wapiga kura wa Bangladesh waliidhinisha pia mageuzi makubwa ya kidemokrasia kupitia kura ya maoni, mageuzi ambayo ni nguzo kuu ya ajenda ya uongozi wa mpito wa Yunus ulioundwa baada ya vuguvugu la umma.

Waraka huo mrefu wa mageuzi, unaojulikana kama "Mkataba wa Julai" unapendekeza mipaka ya mihula kwa mawaziri wakuu, kuundwa baraza la juu la bunge, mamlaka ya urais yenye nguvu na uhuru mkubwa zaidi kwa mahakama.../