Araghchi: Iran haiogopi mazungumzo, wala vita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130398-araghchi_iran_haiogopi_mazungumzo_wala_vita
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema Jamhuri ya Kiislamu haiogopi kuingia katika mazungumzo mapya kuhusu utatuzi wa masuala yoyote yaliyopo, kama ambavyo haina hofu ya kuingia katika vita vyovyote vipya ambavyo vinaweza kutwishwa nchi hii na maadui zake.
(last modified 2025-09-04T07:44:06+00:00 )
Sep 04, 2025 07:44 UTC
  • Araghchi: Iran haiogopi mazungumzo, wala vita

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema Jamhuri ya Kiislamu haiogopi kuingia katika mazungumzo mapya kuhusu utatuzi wa masuala yoyote yaliyopo, kama ambavyo haina hofu ya kuingia katika vita vyovyote vipya ambavyo vinaweza kutwishwa nchi hii na maadui zake.

Araghchi aliyasema hayo katika mahojiano jana Jumatano baada ya kuhimitisha safari aliyoandamana na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran nchini China. "Hatuna hofu ya mazungumzo, kama vile hatuna hofu ya vita," amesisitiza mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran.

Matamshi hayo yametolewa katika hali ambayo, Marekani inadai kuwa ina nia ya kuingia katika mazungumzo mapya na Jamhuri ya Kiislamu.

Araghchi amesema Tehran haijaondoa kabisa matarajio ya kujiunga na mchakato mpya wa kidiplomasia, lakini imeonya, wakati huo huo, kwamba haiwezi kuamini kwa urahisi Washington kutokana na historia ya mwisho ya usaliti.

Maafisa wa Iran wamesema Marekani haiminiki kwa hatua yake ya kujiondoa kinyume cha sheria na kwa upande mmoja katika Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA), mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015, katika muhula wa kwanza wa Donald Trump.

Vile vile wamesema kingine kinachoifanya Tehran isiiamini kiwepesi washington na hatua ya utawala ulio madarakani wa Trump kuupa utawala wa Israel uungwaji mkono wa kisiasa, kijeshi na kijasusi ambao haujawahi kushuhudiwa, wakati wa vita visivyo na msingi vya Tel Aviv dhidi ya Iran mwezi Juni, na pia Washington kujiunga na vita hivyo kwa kushambulia vituo vya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwingineko katika matamshi yake, Araghchi amebainisha kuwa, mipango ya pamoja inaendelea kushughulikia namna nchi hii iyakavyojibu juhudi za mataifa ya Ulaya katika kutumia kile kinachoitwa utaratibu wa snapback wa kulirejeshea taifa hili vikwazo vya Umoja wa Mataifa.