Waziri Zarif afanya mazungumzo na Rais wa Uturuki mjini Ankara
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Muhammad Javad Zarif amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki huko mjini Ankara katika safari ya kwanza muhimu kufanywa na ujumbe wa ngazi za juu wa kigeni tangu lilipotokea jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini humo.
Baada ya mazungumzo na mwenzake wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alishiriki katika Sala ya Ijumaa pamoja na Rais Erdogan na hatimaye kufanya mazungumzo na kiongozi huyo katika Ikulu ya Rais.
Kabla ya mazungumzo yake na Rais wa Uturuki, Dakta Zarif alieleza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na mwenzake wa Uturuki kwamba kupambana na ugaidi, misimamo ya kufurutu mpaka na mielekeo ya kimapote ni malengo ya pamoja ya Tehran na Ankara.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema kuwa Tehran inakaribisha kuwepo uhusiano wa karibu baina ya Uturuki na Russia na kuongeza kuwa kwa kuondoa baadhi ya vizuizi ushirikiano wa Tehran na Ankara pia katika sekta za umeme, nishati pamoja na utalii utastawishwa zaidi.
Dakta Zarif alifafanua kuwa:"Japokuwa tunahitilafiana kimawazo katika baadhi ya masuala lakini tuna mtazamo wa pamoja kuhusu umoja wa ardhi ya Syria na kwamba kuna ulazima wa kupambana na Daesh, Jabhatu-Nusra na makundi mengine ya kigaidi".
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu amesifu na kupongeza misimamo ya Iran ya kuiunga mkono serikali ya nchi hiyo na kueleza kwamba:" Katika muda uleule wa kutokea jaribio la mapinduzi ya kijeshi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alieleza kupitia mawasiliano kadhaa ya mazungumzo kwa njia ya simu uungaji mkono wake kwa serikali na wananchi wa Uturuki dhidi ya wafanya mapinduzi".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alifanya safari ya siku moja nchini Uturuki hapo jana ambapo pamoja na mambo mengine ililenga kuchunguza mwenendo wa matukio na ushirikiano wa pande mbili pamoja na masuala ya kieneo na kimataifa.../