"Israel haiaminiki; Iran inaunga mkono kusimamishwa mauaji ya kimbari Gaza"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131886-israel_haiaminiki_iran_inaunga_mkono_kusimamishwa_mauaji_ya_kimbari_gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema Jamhuri ya Kiislamu inakaribisha kusitishwa kwa mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza, huku akitoa indhari juu ya tabia ya kutokuwa na muamana Tel Aviv kwa kukiuka makubaliano kadhaa ya huko nyuma.
(last modified 2025-10-12T02:59:00+00:00 )
Oct 12, 2025 02:59 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema Jamhuri ya Kiislamu inakaribisha kusitishwa kwa mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza, huku akitoa indhari juu ya tabia ya kutokuwa na muamana Tel Aviv kwa kukiuka makubaliano kadhaa ya huko nyuma.

Araghchi ameyasema hayo katika mahojiano ya kina ya televisheni jana Jumamosi, akizungumzia hatua ya hivi karibuni ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas ya kukubali kutekelezwa kwa awamu ya kwanza ya mpango wa kusitisha mapigano unaolenga kukomesha mauaji ya kimbari ya zaidi ya miaka miwili Gaza.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema Tehran siku zote imekuwa ikiunga mkono mpango wowote na hatua yoyote ambayo ingepelekea kukomesha uhalifu wa Wazayuni dhidi ya watu wa Gaza, na kukomesha mauaji haya ya kimbari.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, hakuna mtu ambaye haungi mkono ukweli kwamba jinai zote hizi, mauaji haya yote ya kimbari na uharibifu unaofanywa dhidi ya Gaza, lazima yakomeshwe.

Wakati huo huo, Araghchi ameashiria ujumbe wa Israel kwa Iran uliowasilishwa na Rais wa Russia, Vladimir Putin hivi karibuni, ambapo utawala huo wa Kizayuni ulidai kuwa hautaki vita na Jamhuri ya Kiislamu na kueleza kuwa: Hatua ya utawala huo kushambulia ardhi ya Iran, ikiwemo wakati wa vita vya Tel Aviv visivyo na msingi na haramu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu mwezi Juni ni mfano wa wazi wa kutoaminika Israel.

Kwingineko katika matamshi yake, Araghchi amemhutubu Rais Donald Trump wa Marekani kujaribu kufungamanisha masuala hayo ya kieneo na suala la mazungumzo kuhusu mpango wa nishati ya nyuklia wa Iran. Amepuuzilia mbali kuwepo uhusiano wowote kati ya mambo hayo mawili.

"Siku zote tumesema kwa uthabiti kwamba, mazungumzo yetu yanahusu suala la nyuklia pekee," Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza.