Araqchi afanya mazungumzo na wenzake wa Msumbiji na Mali mjini Kampala
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i132118-araqchi_afanya_mazungumzo_na_wenzake_wa_msumbiji_na_mali_mjini_kampala
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Msumbiji na Jamhuri ya Mali wamekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pambizoni mwa Kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM mjini Kampala, Uganda.
(last modified 2025-10-18T04:35:01+00:00 )
Oct 18, 2025 04:35 UTC
  • Araqchi afanya mazungumzo na wenzake wa Msumbiji na Mali mjini Kampala

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Msumbiji na Jamhuri ya Mali wamekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pambizoni mwa Kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM mjini Kampala, Uganda.

Katika mazungumzo kati ya Seyyed Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Maria Manuela de Santos Lucas, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Msumbiji wawili hao walijadili na kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa pande mbili kati ya Tehran na Maputo na matukio ya kieneo na kimataifa.

Mawaziri hao wawili walieleza utayari wa nchi zao wa kuimarisha mawasiliano katika ngazi mbalimbali ili kupanua ushirikiano.

Pande hizo mbili pia zimejadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya ajenda ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote hususan haja ya kuwepo ushirikiano na mshikamano baina ya nchi wanachama ili kukabiliana vilivyo na sera za uchukuaji maamuzi ya upande mmoja na ukiukaji wa mara kwa mara wa sheria katika ngazi ya kimataifa na pia suala la Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Aidha Sayyid Abbas araqchi alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop. Wawili hao walibadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa pande mbili na kujadili njia za kupanua uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Umuhimu wa kukuza mshikamano na ushirikiano baina ya nchi wanachama wa Jumuiaya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM, kulinda haki na maslahi ya nchi za Kusini mwa dunia, suala la Palestina na ushirikiano wa Iran na Afrika ni miongoni mwa mada zilizojadiliwa na Mawaziri hao wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Mali.