Maonesho ya 16 ya Teknolojia ya Nano ya Iran yafanyika Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i132826-maonesho_ya_16_ya_teknolojia_ya_nano_ya_iran_yafanyika_tehran
Maonesho ya 16 ya Teknolojia ya Nano ya Iran yamefanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Kimataifa jijini Tehran, yakileta pamoja zaidi ya kampuni 150 za kiteknolojia.
(last modified 2025-11-05T13:24:36+00:00 )
Nov 05, 2025 12:36 UTC
  • Maonesho ya 16 ya Teknolojia ya Nano ya Iran yafanyika Tehran

Maonesho ya 16 ya Teknolojia ya Nano ya Iran yamefanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Kimataifa jijini Tehran, yakileta pamoja zaidi ya kampuni 150 za kiteknolojia.

Tukio hilo, lililoanza tarehe 2 Novemba na kuhitimishwa leo, lililenga kuendeleza biashara ya bidhaa za teknolojia ya nano, kuwezesha ushiriki wa kampuni za maarifa au knowledge-based katika masoko ya kimataifa, na kuimarisha mahusiano yao na vituo vya utafiti, wawekezaji, na makampuni makubwa.

Kwa sasa, kampuni 400 zinajishughulisha na teknolojia ya nano nchini Iran, zikiwemo zile zinazofanya kazi katika sekta za tiba, mazingira, na nishati. Kampuni hizi zina mchango mkubwa katika kukuza teknolojia bunifu na kuongeza uwezo wa ushindani wa taifa.

Maonesho haya ya 16 yameangazia hasa bidhaa bunifu katika nyanja za tiba, kilimo, viwanda, nishati, mazingira, usafiri, uhandisi wa majengo, nguo, na vifaa vya teknolojia ya hali ya juu.

Iran imepiga hatua kubwa katika teknolojia ya nano ndani ya mwaka mmoja uliopita, ikiwa na ongezeko la zaidi ya asilimia 100 katika mauzo ya bidhaa za nano nje ya nchi, kuorodhesha makala 10,860 katika hifadhidata ya Web of Science (WoS), na kushika nafasi ya sita duniani kwa idadi ya makala za teknolojia ya nano.

Kwa kuchapisha jumla ya makala 4,615 katika majarida ya kiwango cha juu (Q1) mwaka 2024, Iran imeorodheshwa miongoni mwa nchi kumi bora duniani kwa uchapishaji wa makala za teknolojia ya nano, na kushika nafasi ya 12 duniani kwa h-index ya makala za nano.