Gharibabadi: Uhusiano imara wa Iran na Saudi Arabia utaleta manufaa makubwa
-
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi (kushoto), akiwa mkuu wa ujumbe wa Iran, anakutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi, Abdulrahman al-Rassi (kulia) mjini Riyadh katika tarehe ambayo haikutajwa.”
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kimataifa na kisheria, Kazem Gharibabadi, amesisitiza umuhimu wa kistratejia wa kurejeshwa kwa uhusiano na Saudi Arabia, akisema kuwa kuimarika kwa mahusiano ya kirafiki kati ya Tehran na Riyadh ni kwa faida za pande mbili na pia ni nguvu muhimu ya kuimarisha uthabiti wa eneo na amani ya kimataifa.
Gharibabadi ametoa kauli hizo kupitia ukurasa wake wa X, kufuatia ziara nchini Saudi Arabia iliyolenga kuendeleza ushirikiano na uratibu kati ya mataifa hayo mawili yenye uzito mkubwa katika eneo.
Naibu waziri huyo amesisitiza kuwa Iran na Saudi Arabia, ambazo zina maslahi mengi ya pamoja na zinaheshimiana, ziko katika nafasi nzuri kuhudumia manufaa ya watu wao na kusukuma mbele amani ya kikanda.
Amefafanua kuhusu mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia anayeshughulikia Masuala ya Kimataifa, Abdulrahman al-Rassi.
Amesema mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano ndani ya taasisi za kimataifa, za kikanda na kimataifa za pande nyingi, pamoja na kusukuma mbele maeneo muhimu kama haki za binadamu na ushirikiano wa kisheria na kimahakama.
Wanadiplomasia hao pia walibadilishana mawazo juu ya kuimarisha nafasi ya msingi ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).
Gharibabadi amesisitiza haja ya OIC kuwa na sauti thabiti zaidi katika kukabili masuala muhimu, ikiwemo kulaani uhalifu wa utawala wa Israel huko Gaza na mashambulizi yake katika eneo, sambamba na kupanua ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama.
Afisa huyo wa Iran ameonyesha matumaini kuhusu mwelekeo wa siku zijazo wa uhusiano wa Tehran na Riyadh, akidokeza hamu ya kasi zaidi na ubora katika maendeleo ya mahusiano.
Iran na Saudi Arabia zilirejesha uhusiano wao kupitia makubaliano yaliyosimamiwa na China mjini Beijing mwezi Machi 2023.
Hatua hii mpya ya kidiplomasia inaonekana kuwa mwanzo wa mfumo thabiti zaidi wa usalama wa kikanda unaosimamiwa na mataifa ya eneo badala ya kutegemea madola ajinabi.