Kwa nini kilio cha machungu ya Wapalestina hakisikiwi na walimwengu?
Hakuna usiku mtulivu huko Gaza, si kabla ya kusitishwa kwa mapigano au baada ya tangazo la amani na usiitishaji vita la Sharm el-Sheikh nchini Misri.
Mtandao wa Middle East Eye hivi karibuni ulichapisha makala ya mwandishi habari Lubna Masarwa na sehemu ya makala hiyo ilisema: Wakati viongozi wa dunia katika eneo la mapumziko la pwani ya Sharm el-Sheikh la Misri walipokuwa wakitabasamu na kupeana mikono kwa bashasha na Rais Donald Trump wa Marekani, wakizungumzia kumalizika vita na mapigano huko Gaza, jeshi la Israel liliendelea kushambulia kwa mabomu Ukanda huo bila kuacha; ni kana kwamba eneo hilo halikupumua.
Kwa mujibu wa Pars Today, utawala wa Kizayuni uliwaua zaidi ya raia 104 wa Palestina siku moja tu baada ya kusitishwa mapigano wakiwemo watoto 46 na watu 18 wa familia moja. Wengi wa wahanga na waathiriwa hata hawakuwa hata na majina; waliuawa shahidi kimya kimya na bila kujulikana.
Kwa ulimwengu, Wapalestina si wanadamu tena; wamekuwa viumbe wasio na hisia, wasio na historia, wasio na hadithi, na wasio na mustakabali. Wakati vyombo vya habari vya Israel vikiandika simulizii za maisha ya mateka wao kwa undani, kuanzia vyakula wanavyovipenda hadi wanaporejea kwa familia zao, hakuna anayetokwa machozi kwa watoto waliouawa shahidi wa Gaza.
Siku ya kusitisha mapigano, televisheni ya utawala wa kizayuni ya Israel ilitangaza tukio ambalo mke wa mateka wa Israel alimwamsha mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitano na kumwambia kwamba, babake amerejea. Watangazaji wa televisheni walikuwa wakitokwa na machozi ya hisia ya furaha.
Lakini siku hiyo hiyo, jeshi la utawala ghasibu Israel lilivamia nyumba za familia za wafungwa wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi ambao walikuwa karibu kuachiliwa. Familia zilitishiwa kwamba, hazina haki ya kushangilia na kufurahikia, hata ikiwa wapendwa wao wataachiliwa huru.
Razan, binti wa mfungwa wa Kipalestina, alisema: “Askari walishambulia nyumba yetu, wakatutisha na hata hawakumruhusu mtu yeyote kumpongeza baba yangu.” Katika shambulio hilo hilo, kijana mmoja alijeruhiwa na wengine kadhaa kupigwa vibaya.
Huko Gaza, Haitham Salim, mfungwa wa Kipalestina aliyeachiliwa huru, alifahamu baada ya kuachiliwa kwake kuwa mkewe na watoto wake watatu waliuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel. Akiwa hospitalini, alisema huku akililia na kububujikwa na machozi: “je wanangu wako hai? Hapana... wamekufa. Siku ya kuadhimisha kuzaliwa binti yangu ilikuwa baada ya siku nne.” Haithamn aliinua bangili aliyomtengenezea binti yake gerezani na kusema: “Nilimtengenezea bangili hii kwa mikono yangu mwenyewe.”
Binti yake alikuwa na umri sawa na mtoto wa mateka wa Israeli ambaye alikuwa amesherehekea sherehe ya kuzaliiwa siku chache zilizopita. Lakini kwa Salim, hakuna machozi yaliyomwagika kwa ajili yake, na hakuna mtu aliyebakia kwa ajili ya kumpokea na kumkaribisha.
Wakati Israel inaendelea kuzungumza kuhusu "haki ya kujilinda," hakuna anayetetea watu wa Gaza au Ukingo wa Magharibi. Hata maisha ya zaidi ya Wapalestina 68,000, wakiwemo watoto 20,000, hayajatoshi kwa ulimwengu kuonyesha radiamali na hisia za majonzi.
Kwa usiku mmoja, mabomu ya Israeli yanaweza kuua mamia ya watu. Israel inaijulisha tu Marekani kabla ya kushambulia, na siku inayofuata, "kusitishwa mapigano" kunatangazwa tena, kabla hata miili ya watoto haijazikwa.
Serikali zilizotia saini Azimio la Sharm el-Sheikh zinawashauri Wapalestina kwamba njia pekee ya kupata uhuru ni mazungumzo, na sio muqawama na mapambano. Lakini Israel imeonyesha kwamba haitaheshimu wala kufungamana na makubaliano ya aina yoyote na historia imethibitisha hilo kivitendo.
Mtindo mpya wa "baada ya vita" unachukua sura, mtindo ambao umebuniwa na Israel na kuidhinishwa na viongozi wa Kiarabu na Kiislamu kwa matabasamu, bashasha na kupeana kwao mikono na Trump muungaji mkono mkuu wa Israel inayofanya mauaji kila uchao dhidi ya Wapalestina.
Katika mtindo huu, "haki ya kujihami" imebadilishwa na kuchukkua nafasi ya "haki ya kujibu," ambayo kivitendo ina maana ya kutoa leseni na idhini ya kudumu ya kuua Wapalestina wakati wowote Israel inapotaka kufanya hivyo.