Kwa nini vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran vimefeli?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133038-kwa_nini_vikwazo_vya_mafuta_dhidi_ya_iran_vimefeli
Shirika la Kimataifa la Ufuatiliaji wa Meli za Mafuta, katika ripoti yake mpya, limesema kuwa mauzo ya nje ya mafuta ghafi ya Iran yamefikia kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miaka saba iliyopita.
(last modified 2025-11-16T06:33:27+00:00 )
Nov 11, 2025 03:19 UTC
  • Meli ya kubeba mafuta
    Meli ya kubeba mafuta

Shirika la Kimataifa la Ufuatiliaji wa Meli za Mafuta, katika ripoti yake mpya, limesema kuwa mauzo ya nje ya mafuta ghafi ya Iran yamefikia kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

Shirika hilo linalojulikana kama Tanker Trackers limetangaza kwamba, katika mwezi wa Septemba 2025, mauzo ya mafuta ghafi ya Iran yalifikia takribani mapipa milioni 2 kwa siku, idadi ambayo haijawahi kufikiwa tangu katikati ya mwaka 2018. Kupitia ujumbe wake katika mtandao wa X, lilisema kuwa kiwango hiki ni rekodi mpya tangu mwaka huo.

Takwimu hizi zinatolewa huku vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambavyo Iran huvitaja kuwa ni “batili na vya kidhalimu”, vikirejeshwa tena mwezi Septemba 2025. Marekani na washirika wake wa Ulaya walitarajia kuwa kurejeshwa kwa vikwazo hivyo kutakata mauzo ya mafuta ya Iran katika masoko makuu kama China, lakini taarifa mpya pamoja na uchambuzi wa wataalamu na maafisa wa Iran, zinaonyesha kuwa vikwazo hivyo havikuwa na athari yoyote.

Waziri wa Mafuta wa Iran, Mohsen Pak-Nezhad, awali alisema kuwa kurejea kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa hakutaleta shinikizo jipya dhidi ya mauzo ya nje ya mafuta ya Iran. Akikumbusha uzoefu wa miaka iliyopita, aliongeza kuwa Iran tayari imeweza kuvuka baadhi ya vikwazo magumu zaidi vya Marekani katika sekta ya mafuta.

Balozi wa China nchini Iran, Zhong Peiwu, naye alisisitiza kuwa mahusiano kati ya Iran na China hayatayumbishwa na hatua za Marekani. Alisema: “Tutaendelea kushirikiana kwa nguvu, na hatutaruhusu vikwazo kuharibu mwenendo wa kazi zetu.” Akaongeza kuwa China, kama rafiki wa Iran, haitaacha kuiunga mkono.

Mapipa ya mafuta

Zhong Peiwu alifafanua zaidi kuwa China haikubaliani na shinikizo lisilo la msingi kutoka Marekani, na itapinga hatua hizo kwa vitendo, kuhakikisha kuwa mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya mataifa hayo mawili hayaingiliwi.

Katika miaka ya karibuni, vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran mara nyingi havikufanikiwa, kwa sababu Iran imeweza kutumia njia mbadala, kiufundi, kidiplomasia na kioperesheni, ili kuendelea kuuza mafuta. Ushirikiano na mataifa huru, pamoja na masoko makuu kama China, umesaidia kupitisha mafuta ya Iran licha ya vikwazo. Aidha, China, India na baadhi ya nchi za Kiarabu hazitambui vikwazo vya upande mmoja vya Marekani, na bado zinaendelea kununua mafuta kutoka Iran.

Soko la dunia linahitaji mafuta ya Iran, kwani licha ya vikwazo, Iran bado ni mhusika muhimu katika usambazaji wa nishati. Uwezo wa kuuza mapipa milioni 2 kwa siku mwezi Septemba 2025 unaonyesha hadhi hiyo.

Kadiri miaka inavyopita, uhusiano wa kiuchumi kati ya Iran na mataifa huru umeongezeka. China imepuuza vikwazo vya Marekani na inaona mafuta ya Iran kama sehemu ya mkakati wake wa nishati. Vilevile, ushirikiano wa kiuchumi na kimkakati kati ya Iran na Urusi umeimarika, jambo linalopunguza utegemezi kwa Magharibi.

Nchi nyingi barani Afrika, Amerika ya Kusini na Asia zinatafuta vyanzo vya nishati vya bei nafuu na vya kuaminika; kwao, Iran ni mshirika anayefaa. Pamoja na vikwazo, Iran imehifadhi na hata kuendeleza miundombinu ya uzalishaji na uchenjuaji mafuta.

Iran ina nafasi maalum kwenye soko la kimataifa la nishati, ikiwa na akiba ya nne kwa ukubwa ya mafuta duniani, na ya pili ya gesi asilia. Nafasi yake ya kijiografia, upatikanaji wa Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman, na ukaribu na masoko ya Asia, inaipa uwezo mkubwa wa kuuza mafuta kwa mataifa mbalimbali.

Kwa hivyo, vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran mwaka 2025 vimeshindwa, kwa sababu Iran imetumia umahiri wa kiufundi, busara ya kidiplomasia, na mbinu za kibiashara kudumisha na hata kuongeza mauzo yake. Hii ni dalili ya nguvu ya uchumi wake, uerevu wa kimkakati, na uzito wa kisiasa na kijiografia katika soko la nishati duniani.

Kwa kuangazia mafanikio ya sera za kigeni za Iran, ongezeko la wanunuzi, na ujuzi wa kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na nchi za Magharibi, Iran imeweza kuimarisha nafasi yake katika soko la kimataifa la nishati.