Mahakama ya Iran kuwaadhibu vikali wahusika wa machafuko
Mahakama ya Iran imesema itawafikisha mahakamani watu wote waliohusika katika kusababisha vifo vya watu wakati wa machafuko ya hivi karibuni nchini kote, ikiahidi adhabu kali kwa watakaopatikana na hatia.
Msemaji wa Idara ya Mahakama ya Iran, Asghar Jahangir amesema hayo leo Jumapili na kuongeza kwamba, kesi tayari zimefunguliwa kwa wale walioongoza ghasia zilizokumba miji kadhaa ya Iran wiki iliyopita. Ameongeza kuwa, maficho ya viongozi hao yametambuliwa, na baadhi yao yamefungwa.
"Idara ya Mahakama bila shaka itatoa adhabu kali kwa wale wote waliochochea ghasia hizo, adhabu ambayo itawafanya wajutie vitendo vyao," msemaji huyo wa mahakama amesema hayo wakati wa mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari hapa Tehran.
"Yeyote anayehusika katika kusababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali za umma na za kibinafsi atawajibishwa," amesisitiza Jahangir ambapo pia amewapongeza wananchi wa Iran kwa msimamo thabiti dhidi ya ghasia hizo za hivi karibuni.
Amesema kwamba Wairani, kupitia maandamano yao ya watu zaidi ya milioni moja kote nchini Jumatatu iliyopita, walionyesha kuwa wako macho na kuwathibitishia maadui na marafiki zao ndani ya nchi kwamba wanaunga mkono kwa dhati mfumo wa Kiislamu.
Machafuko yalizuka katika miji kadhaa ya Iran wiki iliyopita baada ya vikundi vya kigaidi, vikiungwa mkono na wahusika wa kigeni ikiwa ni pamoja na Marekani na Israel, kuteka nyara maandamano ya amani ambayo yalikuwa yameanza siku chache zilizopita kuhusu masuala ya kiuchumi.
Maandamano hayo yalibadilika na kuwa matukio ya vurugu wakati ambapo serikali ya Iran ilikuwa katika mazungumzo na wawakilishi wa waandamanaji ili kusikiliza madai yao.