Iran: Maadui wajiandae kwa 'jibu la uharibifu' wakituchokoza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136014-iran_maadui_wajiandae_kwa_'jibu_la_uharibifu'_wakituchokoza
Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Iran ameonya kwamba, hatua yoyote ghalati dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu itawasababishia maadui uharibifu mkubwa, akisisitiza kwamba vitisho dhidi ya Tehran kupitia maonyesho ya kijeshi havilishughulisha taifa hili.
(last modified 2026-01-29T03:48:45+00:00 )
Jan 29, 2026 03:48 UTC
  • Iran: Maadui wajiandae kwa 'jibu la uharibifu' wakituchokoza
    Iran: Maadui wajiandae kwa 'jibu la uharibifu' wakituchokoza

Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Iran ameonya kwamba, hatua yoyote ghalati dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu itawasababishia maadui uharibifu mkubwa, akisisitiza kwamba vitisho dhidi ya Tehran kupitia maonyesho ya kijeshi havilishughulisha taifa hili.

Admeli Habibollah Sayyari, Naibu Mratibu Mkuu wa Jeshi la Iran aliyasema hayo jana Jumatano na kuongeza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu inakabiliwa na vita mseto na vya utambuzi, akirejelea hatua ya hivi karibuni ya Marekani ya kupeleka manowari na meli za kubeba ndege katika Ghuba ya Uajemi.

Sayyari amesema Washington imekuwa ikifuatilia diplomasia ya manowari na vitisho tangu 1980, akielezea kwamba kupelekwa kwa meli kubwa za majini na vifaa vingi vya kijeshi kunalenga kuwatishia washindani wa Marekani na kuonyesha uwezo wa kusababisha uharibifu.

Admeli Sayyari ameonya kwamba, kupelekwa kwa meli za kijeshi hakupaswi kuwapotosha wafanya maamuzi, akisisitiza kwamba ikiwa tukio lolote litatokea, upande wa pili pia utapata uharibifu, na kwamba uharibifu huo utakuwa mkubwa.

Kamanda huyo pia amesema Jeshi la Iran liko tayari kikamilifu kulinda ardhi, uhuru, mamlaka ya kujitawala na mfumo wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu, sanjari na kujitolea kwake kutimiza misheni na operesheni zake.

Naibu Mratibu Mkuu wa Jeshi la Iran amesema, Jeshi la Iran liko tayari muda wote kukabiliana na vitisho kutoka nchi kavu, baharini, au angani, akisisitiza kwamba Iran imesimama imara na itaendelea kusimama kidete bila kutetereka.

Naye Brigedia Jenerali Seyyed Majid Mousavi, kamanda wa Kitengo cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema, Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali na la haraka kwa vitisho na matamshi ya Marekani, akirudia matamshi yaliyotolewa na maafisa mbalimbali wa Iran kuhusu uwezekano wa kuanzishwa chokochoko mpya za kijeshi na Washington.