IRGC: Iran imepata uwezo mpya wa kukabiliana na maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138688-irgc_iran_imepata_uwezo_mpya_wa_kukabiliana_na_maadui
Afisa mmoja mwandamizi wa kijeshi ameonya kwamba uchokozi wowote mpya wa kijeshi dhidi ya Iran utasababisha jibu la aina tofauti na lenye nguvu zaidi, “lisilofanana na chochote walichowahi kukiona hapo kabla.”
(last modified 2026-05-28T04:50:51+00:00 )
May 28, 2026 04:49 UTC
  • IRGC: Iran imepata uwezo mpya wa kukabiliana na maadui

Afisa mmoja mwandamizi wa kijeshi ameonya kwamba uchokozi wowote mpya wa kijeshi dhidi ya Iran utasababisha jibu la aina tofauti na lenye nguvu zaidi, “lisilofanana na chochote walichowahi kukiona hapo kabla.”

Ali Naderi, Naibu wa Mahusiano ya Umma wa Kikosi cha Anga za Juu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ameoa kauli hizo katika kipindi cha televisheni kilichorushwa kupitia Chaneli ya 3 ya IRIB.

Naderi amesema: “Iwapo maadui wataanzisha tena vita, mbinu ya Jamhuri ya Kiislamu katika kukabiliana nao itakuwa tofauti na yale waliyoshuhudia hadi sasa, na watakumbana na sura mpya ya uwezo wa mapambano wa Iran katika medani ya vita.”

Amesema kuwa Iran sasa imekuwa imara zaidi na yenye maandalizi makubwa zaidi katika nyanja za mashambulizi na ulinzi ikilinganishwa na hapo awali, kwa kutegemea mafunzo yaliyopatikana wakati wa vita vya pili na vya tatu vya kulazimishwa vilivyoanzisha na Marekani kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel Juni mwaka jana na Februari mwaka huu.

Aidha, amesema kwamba katika vita vya tatu vya kulazimishwa, idadi ya wanajeshi waliouawa shahidi ndani ya vituo vya kijeshi ilipungua kwa kiwango kikubwa.

Naderi pia amesema kwamba katika vita hivyo vya tatu vya kulazimishwa, sehemu ya silaha za kisasa na zana za kijeshi za adui ziliangukia mikononi mwa Iran.

Amesema kwa kutegemea silaha zilizoundwa ndani ya nchi na wataalamu vijana Wairani, Iran imeilazimisha dola kubwa ya dunia kurudi nyuma.

Aidha afisa huyo wa IRGC amesema viwanda vya uzalishaji wa makombora na droni sasa vinafanya kazi kwa uwezo mkubwa zaidi kuliko hapo awali. Amebaini kuwa moja ya malengo makuu ya Marekani na Israel katika vita vya pili na vya tatu vya kulazimishwa, yaani kuvuruga mistari ya uzalishaji wa makombora na droni ya Iran, hayakuwahi kufikiwa.

Naderi pia amesema kuwa ingawa Iran haitaki kuanzisha vita, kwa mujibu wa mafundisho ya Imam Khomeini na Kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khamenei, taifa hili litasimama kwa nguvu dhidi ya uchokozi wowote.