“Umma wa Mtume” ni Kaulimbiu Kuu ya Wiki ya Umoja wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140938-umma_wa_mtume_ni_kaulimbiu_kuu_ya_wiki_ya_umoja_wa_kiislamu
Katibu wa Makao Makuu ya Wiki ya Umoja wa Kiislamu nchini Iran ametangaza kuwa kaulimbiu kuu ya hafla ya mwaka huu ni “Ummah wa Mtume Mtukufu (SAW).”
(last modified 2026-08-25T03:16:01+00:00 )
Aug 25, 2026 03:14 UTC
  • Hujjatul-Islam Hassan Akhtari
    Hujjatul-Islam Hassan Akhtari

Katibu wa Makao Makuu ya Wiki ya Umoja wa Kiislamu nchini Iran ametangaza kuwa kaulimbiu kuu ya hafla ya mwaka huu ni “Ummah wa Mtume Mtukufu (SAW).”

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Tehran siku ya Jumatatu, Hujjatul-Islam Hassan Akhtari alifafanua programu mbalimbali zilizopangwa kwa ajili ya wiki hii adhimu.

Akirejelea umuhimu wa umoja wa Ummah wa Kiislamu, alisema kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu, ikizingatiwa kuwa moja ya nguzo na kanuni muhimu za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni umoja wa Waislamu.

Huku akitoa salamu za kheri na fanaka kwa  kuingia kwa mwezi wa Rabi’ al-Awwal na matukio ya mwezi huu, ikiwemo Milad un Nabii, yaani kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu Muhammad (SAW), amesema kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni fursa ya kuimarisha mshikamano na udugu miongoni mwa Waislamu ulimwenguni kote.

Katibu huyo wa Makao Makuu ya Wiki ya Umoja wa Kiislamu ameongeza kuwa Imam Khomeini (RA) pia alichukulia suala la umoja wa Ummah wa Kiislamu kama moja ya kanuni za msingi za mfumo tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa kuitangaza Wiki ya Umoja, aliweka msingi thabiti wa mshikamano mkubwa zaidi miongoni mwa Waislamu.

Akirejelea hali ya kikanda na matukio ya sasa, Hujjatul-Islam Akhtari amesema kuwa mwaka huu, Wiki ya Umoja inafanyika wakati ambapo Ummah wa Kiislamu unakabiliwa na machungu na misukosuko mikubwa.

Akibainisha programu zilizopangwa, amesema kuwa hafla kuu itakuwa ni Kongamano la 40 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu, litakalokuwa na mada ya: “Umoja wa Kiislamu katika Fikra za Imam Shahidi Sayyid Ali Khamenei, Bwana wa Mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu.”

Siku ya 17 ya Rabi’ al-Awwal, ambayo mwaka huu inaangukia tarehe 30 Agosti, inaaminika na Waislamu wa Shia kuwa ndiyo kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), wakati Waislamu wa Sunni wanaamini kuwa siku ya 12 ya mwezi huo (Agosti 25 mwaka huu) kuwa ndiyo siku ya kuzaliwa kwa Mtume wa mwisho.

Muda kati ya tarehe hizo mbili ulitangazwa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini, katika miaka ya 1980.