Wanafunzi na wanazuoni wa mji wa Qum waandamana kulaani ukandamizaji Bahrain
Wanafunzi na wanazuoni wa vyuo vikuu vya kidini katika mji wa Qum, kusini mwa mji wa Tehran nchini hapa, wamefanya maandamano kulaani ukandamizaji wa kuchupa mipaka unaofanywa na utawala wa kidikteta nchini Bahrain dhidi ya wananchi wa taifa hilo.
Waandamanaji hao pia wamelaani hatua ya utawala wa Aal-Khalifa ya kumfutia uraia Sheikh Issa Qasim, kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Bahrain. Sanjari na kulaani mwenendo wa kichokozi wa utawala huo dhidi ya Waislamu wa Kishia, wanafunzi hao na wanazuoni wamezitaka taasisi za kimataifa kuchunguza ukandamizaji wa haki za binadamu nchini Bahrain.
Katika mjumuiko huo, Hujjatul-Islamu wal-Musilimina Muhammad Hassan Akhtari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlubaiti na Sheikh Abdullah al-Daqqaq mmoja wa maulama wa Bahran, walitoa hotuba wakielezea ukandamizaji wa kuchupa mipaka unaofanywa na utawala huo wa kidikteta wa Aal-Khalifa nchini Bahrain.
Wakati huo huo Ariyal Blutigen, mratibu wa masuala ya Bahrain katika Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International, amelaani vikali kamatakamata na pia kitendo cha utawala wa nchi hiyo cha kumnyang'anya uraia mwanazuoni mashuhuri wa Bahrain, Sheikh Issa Qasim na kusema kuwa, vitendo hivyo mbali na kwamba ni vya kidhamu, lakini pia vinakinzana na sheria za kimataifa.