Oct 09, 2016 08:08 UTC
  • Iran iko Mstari wa Mbele Kukabiliana na Dawa za Kulevya

Ghulam Hussein Dehqani, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa katika kikao cha Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu dawa za kulevya alisema, zaidi ya asilimia 80 ya ufyuni na zaidi ya asilimia 40 ya heroini inayokamatwa kutoka kwa walanguzi duniani hukampatwa na vikosi vya usalama vya Iran.

Dehqani ameongeza kuwa,  Wairani elfu 12, wakiwamo maafisa usalama, wameuawa shahidi na wengine elfu 12 kujeruhiwa katika mapambanao na wafanya biashara haramu ya dawa za kulevya. Ameongeza kuwa Iran kila mwaka hutumia mamia ya milioni za dola katika vita dhidi ya biashahra haramu ya dawa za kulevya na hivyo kuifanya nchi hii kuwa mstari wa mbele katika mapambano hayo.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Idara ya Kupambana na Mihadarati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mwaka uliopita, maafisa wa usalama nchini waliweza kukamata tani 620 za aina mbali mbali za mihadarati na hii ni idadi kubwa zaidi ya mihadarati iliyowezeka kukamatwa duniani katika kipindi hicho. Kutokana na kuwa Iran inapakana na Afghansitan, nchi ambayo ni mzalisha mkubwa zaidi ya afyuni duniani, iko katika njia inayotumiwa na wale ambao husafirisha mihadarati kuelekea Ulaya. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na hatua zilizochukuliwa na Iran kwa ushirikiano na vikosi vya usalama vya Afghanistan na Pakistan, kumeshuhudiwa kupungua kwa kiasi kikubwa usafirishaji mihadarati kutoka Afghanistan kuelekea katika soko la dunia.

Shamba la maua ya afyuni nchini Afghanistan

Iran imekuwa ikifanya jitihada kubwa katika kukabiliana na mihadarati na kuzuia mada hizo hatari kwa afya ya mwanadamu kufika katika maeneo mengine duniani. Hii ni katika hali ambayo jamii ya Kimataifa haijatoa msaada wowote wa maana kwa Iran katika mapambano dhidi ya mihadarati.

Kwa mujibu wa Abdul Ridha Rahmani Fadhli, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran na ambaye pia ni Katibu wa Idara ya Kupambana na Mihadarati nchini,  Jamhuri ya Kiislamu inaongoza katika vita vya kuangamiza mihadarati duniani lakini haipati himaya  yoyote ya jamii ya kimataifa katika kukabiliana na mihadarati.

Uzalishaji wa mihadarati Afghanistan umeongezeka mara nne zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 tokea nchi hiyo ivamiwe na kukaliwa kwa mabavu na Muungano wa Kijeshi wa NATO unaoongozwa na Marekani. Si tu kuwa jamii ya kimataifa haisaidii Iran katika vita dhidi ya mihadarati bali kinyume na hilo, nchi hii imewekewa vikwazo vilivyo kinyume cha sheria. Vikwazo hivyo vimepelekea Iran isiweze kununua zana muhimu zinazohitajika katika kukabiliana na wafanyabiashara haramu ya mihadarati. Kwa kuzingatia kuwa hivi sasa mihadarati imeanza kusafirishwa kwa wingi kupitia baharani, nchi za Ghuba ya Uajemi zimetoa wito wa msaada wa kutumia uzoefu wa Iran katika vita dhidi ya wanaosafirisha mihadarati. Iran inaongoza kivitendo katika vita dhidi ya uuzaji na utumizi wa mihadarati na hilo limethibitishwa na taasisi za kimataifa.

Ukulima wa mimea ya mihadarati Afghanistan umeongezeka mara nne tokea askari wa Marekani waivamie nchi hiyo

Ni kwa sababu hii ndio Iran inataka dunia ifahamishwe kuhusu harakati za kibinadamu za taifa la Iran kwa watu wa dunia nzima katika vita vyake dhidi ya mihadarati. Hii ni kwa sababu mihadarati inayozalishwa Afghanistan si tu kuwa ni tishio kwa kwa nchi za eneo bali kwa watu wote hasa vijana wa dunia nzima.

Tags