Iran na Bosnia Herzegovina kuimarisha uhusiano
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mwenyekiti wa Baraza la Urais wa Bosnia Herzegovina wamesisitiza kuhusu kuimarishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbali mbali hasa katika sekta ya uchumi.
Hassan Rouhani Rais wa Iran na Bakir Izetbegović Mwenyekiti wa Baraza la Urais wa Bosnia Herzegovina ambaye huko safarini nchini Iran wamefanya mazungumzo leo mjini Tehran. Katika kikao hicho, Rais Rouhani amesema pamoja na kuwa nchi mbili zimekuwa na uhusiano tokea wakati Bosnia ilipopata uhuru, lakini hakuna shaka kuwa safari ya ujumbe wa Bosnia mjini Tehran ni mwanzo mpya katika kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili.
Rais Rouhani amesema katika miaka ya nyuma, kutokana na vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran, uhusiano wa Tehran na Sarajevo ulidorora lakini hivi sasa baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia, kuna mazingira mazuri ya kuboreshwa uhusiano wa pande mbili.
Rais Rouhani ameashiria masuala ya kieneo na kusema ugaidi na misimamo mikali ni hatari kubwa kwa eneo na dunia nzima kwa ujumla. Kwa upande wake Bakir Izetbegović Mwenyekiti wa Baraza la Urais wa Bosnia Herzegovina ameutaja uhusiano wa Tehran na Sarajevo kuwa ni imara na wa kirafiki. Amekumbusha kuwa, wakati wa vita vya Bosnia, Iran ilijitahidi sana kuhitimisha vita hivyo na kurejesha amani na uthabiti. Bakir Izetbegović amesema Bosnia itashirikiana na Iran katika vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali ya kidini.