Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu kufanyika Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i21376-mkutano_wa_kimataifa_wa_umoja_wa_kiislamu_kufanyika_tehran
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema mkutano wa kimataifa wa kila mwaka wa Umoja wa Kiislamu utafanyika wiki hii mjini Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 14, 2016 00:55 UTC
  • Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu kufanyika Tehran

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema mkutano wa kimataifa wa kila mwaka wa Umoja wa Kiislamu utafanyika wiki hii mjini Tehran.

Ayatullah Muhsin Araki amesema mkutano huo ni nembo ya Umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu katika kukabiliana na maadui.

Akizungumza Jumanne mjini Tehran, Ayatullah Araki amesema mkutano huo utaanza Alhamisi na kuendelea kwa muda wa siku tatu. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema mwaka huu kuna vikao vya umoja wa Kiislamu kote Iran na maeneo mengine duniani katika Wiki wa Umoja. Aidha amesema sherehe za Miladun-Nabii na Wiki ya Umoja wa Waislamu mwaka huu zimefanyika kwa mafanikio zaidi ya miaka iliyopita na hili linaonyesha kuimarika umoja wa Kiislamu.

Mkutano wa Umoja wa Kiislamu, Tehran

Ayatullah Muhsin Araki amesema maudhui ya umoja na udharura wa kukabiliana na wimbi la ukufurishaji ni mihimili miwili muhimu ya mkutano ya kimataifa wa Kiislamu wa Tehran mwaka huu. Amesema mkutano huo utahudhuriwa na wasomi 320 wa kitaifa na kimataifa huku akibainisha kuwa magaidi wanaelekea kufeli katika njama yao ya kuanzisha vita vya kimadhehebu baina ya nchi za Kiislamu.

Kwa kauli ya Ahul Sunna, Mtume Muhammad SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal huku Wanachuoni wa madhehebu ya Shia wakiamini alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya Umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa Ulimwengu wa Kiislamu.