Rais wa Iran: Marekani, Israel zinapandikiza chuki baina ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138454-rais_wa_iran_marekani_israel_zinapandikiza_chuki_baina_ya_waislamu
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kwamba tawala za Marekani na Israel zinaendeleza miradi ya kuzusha migawanyiko na kueneza hali ya kutoaminiana ili kuyagonganisha mataifa ya Kiislamu.
(last modified 2026-05-18T13:19:01+00:00 )
May 18, 2026 12:11 UTC
  • Rais Pezeshkian katika kikao na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi
    Rais Pezeshkian katika kikao na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kwamba tawala za Marekani na Israel zinaendeleza miradi ya kuzusha migawanyiko na kueneza hali ya kutoaminiana ili kuyagonganisha mataifa ya Kiislamu.

Akizungumza mjini Tehran katika kikao na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa sera ya msingi ya Iran imejengwa juu ya kuimarisha uhusiano wa kirafiki na mataifa jirani, hususan yale ya mwambao wa Ghuba ya Uajemi.

Amesema kuwa: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka mahusiano ya kirafiki, thabiti na endelevu yanayozingatia ujirani mwema na mataifa ya Kiislamu ya eneo hili. Lakini tawala za Marekani na Israel daima zimekuwa zikijaribu kutekeleza miradi ya kuibua mizozo baina ya mataifa ya Kiislamu.”

Rais Pezeshkian alitoa shukrani kwa nafasi ya Pakistan katika kusimamia mazungumzo ya kusitisha mapigano baada ya siku 40 za vita vya uvamizi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Ameelezea matumaini kuwa juhudi hizo za kidiplomasia zitaleta amani, uthabiti na usalama wa kudumu katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Rais Pezeshkian amelaani mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kuuawa shahidi Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, pamoja na makamanda waandamizi, mawaziri, wanafunzi na raia wasio na hatia. Amesema uhalifu huo mkubwa unakiuka misingi yote ya kibinadamu, kisheria na kimataifa.”

Aidha, amebainisha kuwa Marekani na Israel zimekuwa zikipanga kuingiza makundi ya kigaidi yenye silaha kupitia mipaka ya kaskazini-magharibi na kusini-mashariki mwa Iran.

Hata hivo amesema ushirikiano na uwajibikaji ulioonyeshwa na majirani wa Iran katika kuzuia matumizi mabaya ya ardhi yao dhidi ya Iran ulikuwa hatua ya thamani na ya kupongezwa.”

Rais Pezeshkian pia amezishukuru Pakistan, Afghanistan na Iraq kwa kutoruhusu ardhi zao kutumiwa kufanya vitendo vya uhasama dhidi ya Iran.