Jan 08, 2017 17:08 UTC
  • Ayatullah Hashemi Rafsanjani ameaga dunia

Ayatullah Ali Akbar Hashemi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuanisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu Iran ameaga dunia leo baada ya umri mrefu wa jihadi na jitihada zisizo na kikomo kwa ajili ya Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Hashemi Rafsanjani amepata maradhi ya moyo leo Jumapili usiku mjini Tehran na madaktari wamejitahidi kumpa matibabu ya haraka lakini hawakufanikiwa.

Hashemi Rafsanjani, ambaye ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 82, alijiunga na chuo cha kidini akiwa kijana na kuanza masomo ya kidini hadi kufikia daraja ya Ijtihad.

Tokea mwaka 1958 alijiunga na mapambano dhidi ya utawala wa kiimla  wa Shah ambapo alifungwa jela mara saba na kuendeleza mapambano hayo hadi wakati wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Hayati Ayatullah Rafsanjani

Ayatullah Rafsanjani alikuwa mwenye azma imara katika harakati ya Mapambano ya Kiislamu yaliyoongozwa na Imam Khomeini MA.

Kati ya nyadhifa ambazo Ayatullah Rafsanjani aliwahi kushika baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Kaimu Amri Jeshi Mkuu, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Ulinzi wa Kitaifa na nafasi aliyoishika hadi kifo chake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.

 

 

Tags